MUHIMU KUSOMA;

KARIBU KWENYE SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA OKTOBA 2017.

Habari rafiki? Napenda kuchukua nafasi hii kukupa taarifa za semina ya KISIMA CHA MAARIFA itakayofanyika mwezi oktoba mwaka 2017. Semina ...

Wednesday, January 11, 2017

UCHAMBUZI WA KITABU; THE SLEEP REVOLUTION (Boresha Maisha Yako Kupitia Usingizi Wako)

Posted by Makirita Amani  |  at  Wednesday, January 11, 2017 No comments

Moja ya mahitaji muhimu sana kwenye maisha yetu ni kupata muda wa mwili na akili zetu kupumzika. Mwili unafanya kazi kubwa sana kwenye maisha yetu ya kila siku, na unahitaji pia muda wa kupumzika ili kuweza kuendelea kufanya kazi zaidi kwa siku zinazofuata.
 

Lakini dunia ya sasa imebadilika mno, kumekuwa na mambo mengi ya kufanya kuliko muda tulionao wa kufanya mambo hayo. Na imekuwa ni tabia kwa watu kwamba pale wanapohitaji muda na hawana, basi ipo sehemu moja ya kuiba muda, na sehemu hiyo ni kwenye muda wa kulala, au muda wa usingizi.

Tunaishi kwenye zama ambazo usingizi unaonekana kama ni anasa, kulala ni sawa na kupoteza muda. Kutokana na kasi ya mabadiliko, watu wengi wamepunguza sana muda wa kulala. Licha tu ya mahitaji ya kazi, teknolojia nayo imeingilia sana nafasi yetu ya usingizi. Sasa hivi tunavyo vifaa (simu janja) ambavyo vinatuunganisha na dunia masaa 24 kwa siku. Tunaenda vitandani na vifaa hivi na tukiamka tunavyo. Imefika hatua mtu anachelewa kulala kwa sababu tu anafuatilia mambo yanayoendelea kupitia mtandao wa intaneti.

Mwandishi Arianna Huffington, mwanzilishi wa jarida la Huffington Post, alijifunza thamani na umuhimu wa usingizi kwenye maisha yetu kwa njia ngumu. Alijifunza baada ya kuanguka na kupoteza fahamu ghafla kutokana na kukaa muda mrefu bila ya kupata muda wa kutosha wa kulala.

SOMA; Hatua Sita Za Kubadili Maisha Yako Na Kufikia Mafanikio Makubwa.

Baada ya tukio hili aliamua kufanya utafiti wa kutosha kwenye eneo la usingizi na ndipo akaandika kitabu hiki cha THE SLEEP REVOLUTION. Karibu nikushirikishe yale muhimu niliyojifunza kwenye kitabu hiki.

1. Kuna kiwango cha kuchoka ambapo mtu anakuwa hajui hata kama amechoka, sawa na kiwango cha ulevi ambapo mtu haelewi kama amelewa. Hivi ndivyo dunia ya sasa inavyokwenda, watu wengi wana uchovu na wamekusa muda wa kulala, na hivyo kupeleka siku zao kwa kujisukuma na kushindwa kufanya mambo makubwa.

2. Usingizi ni kitendo ambacho kimekuwa kinaheshimiwa toka enzi na enzi. Kwa sababu huu ndiyo wakati ambao watu waliweza kupumzika na kujiandaa na shughuli za siku inayofuata. Pia ndiyo wakati ambapo watu walipata kuja pamoja. Usingizi pia umekuwa ni wakati wa watu kuota na baadaye kutafsiri maana ya ndoto zao. Hivi ndivyo ilivyokuwa, lakini kwa sasa mambo yamebadilika kabisa.

3. Kwa dunia ya sasa, sehemu rahisi ya kuiba muda ni kwenye usingizi, kupunguza muda wa kulala, pale watu wanapotaka kufanya kazi zaidi, wanapunguza muda wa kulala, pale watu wanapotaka kusoma zaidi wanapunguza muda wa kulala. Hapa tunatengeneza deni ambalo lina madhara makubwa sana kwetu baadaye.

4. Ukweli ni kwamba sehemu kubwa ya watu kwenye jamii zetu hatupati usingizi wa kutosha. Hasa kwa wafanyakazi, wafanyabiashara, wanafunzi na watu wengine ambao wana shughuli mbalimbali. Tumekuwa tunahitaji muda zaidi na sehemu pekee ya kupata muda huo ni kupunguza muda wa kulala, kitu ambacho kinapelekea kupunguza ufanisi wetu, umakini na kuharibu afya zetu.

5. Kwenye jamii nyingi limekuwa linaonekana ni jambo la kishujaa kwa wale ambao wanalala muda mfupi. Watu wamekuwa wakijisifia kabisa, mimi nalala masaa manne tu, au mimi naweza kukesha na mambo yangu yakaenda vizuri. Kwenye jamii nyingi, anayelala mapema anaonekana ni mvivu au hajui anachokitaka, hivyo watu wengi wamekuwa wanajichelewesha kulala huku hakuna la muhimu wanalofanya. Na hata kama wanafanya la muhimu, madhara ya usingizi wanayotengeneza ni makubwa sana.

6. Muda tunaolala siyo muda unaopotea. Ukiangalia kwa haraka unaweza kusema kwamba kulala ni kupoteza muda. Lakini wanasayansi kupitia tafiti wanatuonesha kwamba muda tunaolala kuna mambo mengi yanayoendelea kwenye mwili wetu kwa ajili ya kuufanya kuwa bora zaidi. Ukichukulia mwili kama mfano wa gari, wengi wameuwa wanafikiri kulala ni sawa na kuzima gari, kuna mpaka usemi kwamba kulala ni kuangusha gari. Lakini ukweli ni kwamba kulala ni sawa na gari ambayo imewashwa na kuwekwa gia ambayo ni neutral na hiyo lipo kwenye mngurumo muda wote.

7. Muda tunaolala ndiyo muda ambao mwili na akili zetu zinafanya usafi. Ni muda ambao mwili na akili vinajiandaa kwa ajili ya siku ambayo inafuata. Kama tukichukulia mwili kama betri, basi kulala ndiyo muda w akuchaji betri na unapofanya kazi ndiyo unaitumia betri. Mwisho wa siku betri inakuwa imeisha na inahitaji kuchajiwa tena. Sasa unapochelewa kulala au kukosa usingizi wa kutosha, ni sawa na betri uliyochaji halafu haikujaa, haiwezi kufanya kazi muda mrefu. Ndiyo maana utajikuta unaianza siku yako ukiwa umechoka. Hakikisha unapata muda wa kutosha wa kuchaji betri yako, yaani muda wa kutosha wa kupumzisha mwili na akili yako kupitia kulala.

SOMA; Kanuni Ya Uhakika Ya Kufikia Mafanikio Makubwa Kwenye Maisha Yako. (Hatua Nne Muhimu Za Kufuata).

8. Yafuatayo ni madhara ya kukosa usingizi wa kutosha;

i. Mwili kuwa na uchovu muda wote.

ii. Kupungua kwa kinga ya mwili na kupata magonjwa mara kwa mara.

iii. Kuongezeka kwa uzito wa mwili na kuwa kwenye hatari ya kupata magonjwa kama kisukari na presha.

iv. Kupata msongo wa mawazo na baadaye sonona.

v. Kukosa umakini kwenye kazi na kufanya makosa ya wazi.

vi. Kukasirika haraka kwa mambo madogo.

vii. Kusinzia sehemu ambazo siyo sahihi.

viii. Kupata magonjwa ya akili na kupoteza kumbukumbu.

9. Kukaa masaa 24 bila ya kulala ni sawa na mtu mwenye kilevi cha asilimia 0.1 kwenye mwili wake. Hiki ni kiwango ambacho kisheria huruhusiwi kabisa kuendesha gari au chombo cha moto. Hii ni kwa sababu uwezo wako wa kufanya maamuzi unakuwa umeshuka mno kiasi cha kufanya makosa ya wazi wazi kabisa.

10. Baada ya usingizi kuwa tatizo la msingi kwa watu wengi, watu wameamua kutafuta njia ya mkato ya kutatua tatizo hili na hapa ndipo matumizi ya dawa za usingizi yalipoanza kushika kasi. 
Makampuni ya madawa, hasa kwa nchi zilizoendelea yamenufaika sana na kuwauzia watu dawa za usingizi. Lakini dawa hizi zimekuwa hazitibu tatizo la msingi, badala yake zinatuliza tu dalili za tatizo.

11. Njia nyingine ya mkato ambayo watu wamekuwa wanaitumia kuiba muda mwingi kwenye usingizi ni kutumia vinywaji ambavyo vinachangamsha, vinywaji kama kahawa, au vinywaji vya kuongeza nguvu yaani ENERGY DRINKS kama redbull. Hii ni njia ya kudanganya mwili kwamba haujachoka na hivyo kuendelea kuutumia, lakini gharama yake ni kubwa sana baadaye.

12. Mapinduzi ya viwanda ndiyo yalileta mvurugano mkubwa kwenye utaratibu wa kawaida wa kulala. Ni katika kipindi hiki ambapo wamiliki wa viwanda walipohitaji kupata uzalishaji zaidi kwa kutumia gharama ndogo na hivyo kuja na utaratibu wa kufanya kazi kwa shifti na kwa muda mrefu. Hapa ndipo wafanyakazi walipoanza kufanya kazi kwa zaidi ya masaa 12.

13. Mtazamo wa watu wengi ni kwamba kulala sana ni kupoteza muda. Mvumbuzi Thomas Edison wakati wa uzee wake alipoulizwa kuhusu mtazamo wake kwa maendeleo ya siku za baadaye alisema watu wa siku zijazo watatumia muda mfupi kitandani. Kiongozi wa kivita wa zamani wa ufaransa Napoleon alipoulizwa kuhusu muda wa kulala alijibu, masaa sita kwa mwanaume, saba kwa mwanamke na nane kwa mjinga. Kwa ushawishi wa aina hii kutoka kwa watu waliopita, si ajabu usingizi kuonekana ni kitu cha kupoteza muda.

14. Swali la msingi kabisa ni kwa nini tunalala? Ipi faida ya kulala? Kulala kuna faida nyingi sana kwenye mwili na afya zetu, kulala kunaupa mwili nafasi ya kupumzika, kujitengeneza upya na kuondoa sumu kwenye mwili na akili. Pia kulala kunaupa ubongo nafasi ya kukua. Kwa tafiti za kisayansi inaonesha kwamba ubongo wetu unaendelea kukua licha ya umri tulionao. Zamani iliaminika kwamba mtu akishakua basi ubongo unakoma kukua, lakini si kweli, ukuaji wa ubongo unaendelea kadiri tunavyoupa nafasi ya kukua.

15. Kuna hatua nne za kulala, kila hatua ina umuhimu mkubwa kwenye maisha yetu.
Hatua ya kwanza ni usingizi mwepesi, hili ni daraja kati ya kuwa macho na kuwa umelala. Huu ni ule wakati ambao haupo macho kabisa na pia haupo usingizini.
Hatua ya pili ni usingizi mzito kiasi, hapa macho yanaacha kucheza cheza, joto la mwili linapungua.

Hatua ya tatu ni usingizi mzito ambao una mawimbi ya delta. Huu ni usingizi mzito sana ni siyo rahisi kuamshwa kutoka kwenye usingizi huu. Na ikitokea umeamshwa kwenye hatua hii ya usingizi basi akili yako inakuwa haielewi nini kinaendelea.

SOMA; Viungo Vikuu Vitatu(3) Vya Furaha Ya Kudumu Kwenye Maisha.

Hatua ya nne ni usingizi unaojulikana kama REM SLEEP yaani RAPID EYE MOVEMENT, macho yanakuwa yanacheza cheza. Katika hatua hii ya usingizi ndipo tunapokuwa na ndoto. Mawimbi ya ubongo wakati huu yanakuwa ya kawaida, na ndoto tunazozipata kwenye usingizi huu tunazikumbuka vizuri.

16. Tafiti za kisayansi zinaonesha kwamba ukiipa akili yako jukumu la kufanyia kazi unapokwenda kulala, unaamka ukiwa na majibu au ukiwa na hatua za kuchukua. Hii inaonesha namna ambavyo usingizi ni muhimu kwa maisha yetu ya kawaida.

17. Kukosa usingizi kunahusishwa na kusambaa kwa kazi kwa baadhi ya kansa. Hii inatokana na kupungua kwa kinga ya mwili ambayo inapambana na mabadiliko yanayotokea kwenye mwili. Unapokosa muda wa kulala, kinga yako ya mwili inapungua.

18. Kukosa muda wa kulala pia kunahusishwa na ugumba kwa wanawake na wanaume pia. Kukosa muda wa kutosha wa kulala, kunasababisha uzalishwaji kidogo wa homoni ya testesterone ambayo ndiyo inazalisha mbegu za kiume. Pia kunasababisha kuharibika kwa mpangilio wa homoni mbalimbali za uzazi kwenye mwili wa mwanamke na hivyo kuwa vigumu kubeba ujauzito.

19. Ndoto ni moja ya sehemu muhimu ya usingizi wetu. Kuna maelezo mbalimbali kuhusu ndoto, yapo maelezo kwamba ndoto ni sauti iliyopo ndani yetu ambayo inajua kipi sahihi kufanya lakini huwa hatuipi nafasi na hivyo tunapopumzisha akili zetu sauti hii inapata nafasi. Yapo maelezo kwamba ndoto ni mrejesho wa mambo tuliyofanya kwenye siku yetu au mambo tunayohofia. Kwa vyovyote vile, ndoto zetu ni muhimu na hivyo tunapaswa kuziandika pale tunapoamka na kuona namna tunavyoweza kuzitumia.

20. Swali la msingi kabisa ni je ni muda gani sahihi wa kulala? Yaani muda sahihi kulala ni masaa mangapi? Kutokana na tafiti za kisayansi, muda wa kulala unatofautiana kwa makundi mbalimbali ya watu. Na hapa ni muda kutokana na makundi mbalimbali;

Watoto wachanga (miezi 0 mpaka 3) masaa 14 mpaka 17.

Watoto wa miezi 4 mpaka 11 masaa 12 mpaka 15

Watoto mwaka mmoja mpaka 2 masaa 11 mpaka 14

Watoto miaka 3 mpaka 5 masaa 10 mpaka 13

Watoto miaka 6 mpaka 13 masaa 9 mpaka 11

Watoto miaka 14 mpaka 17 masaa 8 mpaka 10.

Vijana miaka 18 mpaka 25 masaa 7 mpaka 9

Watu wazima miaka 26 mpaka 64 masaa 7 mpaka 9.

Wazee miaka 65 na kuendelea masaa 7 mpaka 8.

Kwa tafiti za kisayansi, huo ndiyo muda sahihi wa kulala ambao ukiweza kuupata unapata manufaa yote yanayotokana na usingizi na kuepuka matatizo yanayotokana na kukosa muda wa kulala.

Weka ratiba zako vizuri ili uweze kupata muda wa kutosha wa kulala, usingizi ni sehemu muhimu ya maisha yetu.

Fanyia kazi haya ambayo umejifunza kwenye uchambuzi wa kitabu hiki ili uweze kuona matokeo bora kwenye maisha yako.

Kupata vitabu vya Kiswahili vya kujisomea ili kuweza kufanikiwa kwenye kazi, biashara na maisha kwa ujumla, tembelea MOBILE UNIVERSITY (www.mobileuniversity.ac.tz)

Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita

KUHUSU AMKA MTANZANIA

AMKA MTANZANIA ni mtandao unaokuhamasisha wewe mtanzania kuchukua hatua juu ya maisha yako. Kupitia mtandao huu utajifunza na kuhamasika ili uweze kuchukua hatua ya kufikia mafanikio makubwa. Kama unataka kutumiwa makala nzuri na vitabu moja kwa moja kwenye email yako, BONYEZA MAANDISHI HAYA na ujaze fomu. KARIBU SANA UJIFUNZE NA KUHAMASIKA

Pata Makala Inapotoka

Weka email yako hapa na uwe wa kwanza kupata makala nzuri inapowekwa kwenye mtandao huu.

Washirikishe Wengine Makala Hii Nzuri

Makala Zinazohusiana na Hii

0 comments:

USIACHE KUWEKA MAONI YAKO HAPA.

© 2013 AMKA MTANZANIA. WP Theme-junkie converted by BloggerTheme9
Blogger templates | Distributed By: BloggerBulk Proudly Powered by Blogger.
back to top