MUHIMU KUSOMA;

KARIBU KWENYE SEMINA YA KISIMA CHA MAARIFA OKTOBA 2017.

Habari rafiki? Napenda kuchukua nafasi hii kukupa taarifa za semina ya KISIMA CHA MAARIFA itakayofanyika mwezi oktoba mwaka 2017. Semina ...

Wednesday, August 17, 2016

UCHAMBUZI WA KITABU; THINK LIKE A CHAMPION (Fikiri Kama Mshindi, Elimu Isiyo Rasmi Kuhusu Biashara Na Maisha.)

Posted by Makirita Amani  |  at  Wednesday, August 17, 2016 2 comments

Donald Trump mwaka huu 2016 anagombea uraisi wa nchi ya marekani. Mengi sana yamesemwa na kuandikwa kuhusu yeye kutokana na namna anavyochukulia mambo na namna anavyoyasema.

Donald Trump ni mtu ambaye amekuwa anasema kile anachojua ni sahihi bila ya kujali wengine wanachukuliaje. Anakataa kitu kinaitwa unafiki hasa kwenye siasa ambapo watu wanatafuta maneno mazuri ya kuongea ili wasiwakasirishe wengine. Kutokana na utayari wake wa kusema mambo kama yalivyo, amekuwa akichukiwa na wengi na pia kupendwa na wengi.

Licha ya kuwa mfanyabiashara na bilionea, Donald Trump pia amekuwa akinadika vitabu. Baadhi ya vitabu vyake ni ART OF THE DEAL, WHY WE WANT YOU TO BE RICH, NEVER GIVE UP na vingine vingi. Leo tutakwenda kuchambua moja ya vitabu vyake kinachoitwa THINK LIKE A CHAMPION. Kuna mengi sana ya kujifunza kupitia kitabu hiki ambacho ni mkusanyiko wa maandiko ya Donald Trump.

Karibu tujifunze kwa pamoja kupitia uchambuzi huu.

1. Huhitaji kuwa mvumbuzi mkubwa au mbunifu sana ili uweze kupata wazo bora la biashara. Badala yake unahitaji kuwa makini na maisha yanayokuzunguka, kuangalia kila ambacho kinaendelea kwenye maisha yako na hii itakupelekea wewe kupata mawazo ya tofauti kuhusu biashara.

2. Kuwa tayari kujifunza na mara zote kuwa tayari kupokea mawazo mapya. Pale unapofikiria na kujiona kwamba unajua kila kitu, ndiyo unakuwa mwisho wako wa kukua na kufanikiwa. Ili kufanikiwa kwenye maisha, ili kuendelea kuwa mbunifu ni muhimu uwe tayari kujifunza kila siku.

3. Usiridhike na mafanikio yoyote unayoyapata, kila hatua unayopiga jua ya kwamba kuna hatua nyingine nyingi zipo mbele yako. unapoanza kuridhika na mafanikio madogo unayopata ndiyo unakuwa mwisho wa mafanikio yako. mara zote weka mipango mikubwa zaidi pale unapofikia ile uliyoiweka mwanzo.

4. Hakuna mafanikio yanayokuja bila ya gharama. Chochote kikubwa unachotaka kwenye maisha yako, jua kuna gharama unayotakiwa kulipa. Jua gharama hiyo na kuwa tayari kuilipa ili uweze kupata kile ambacho unakitaka. Kadiri unavyojua gharama hiyo na kulipa mapema ndivyo unavyoweza kupata mafanikio hayo haraka.

5. Mara zote upo uwezekano wa kushindwa, kwa jambo lolote unalopanga kufanya, hata kama umejiandaa kwa kiasi gani, jua ya kwamba huwezi kuondoa kabisa uwezekano wa kushindwa. Jua upo uwezekano wa kushindwa na hivyo jiandae. Usitake kukutana na kitu chochote kwa mshangao, kuwa na maandalizi.

6. Uaminifu Ni kitu kikubwa na muhimu sana kwenye safari yako ya mafanikio. Watu wanakuwa tayari kufanya kazi na mtu ambaye wanaweza kumwamini. Watu wapo tayari kufanya biashara na mtu ambaye wanamwamini. Kama huna uaminifu, huwezi kufanikiwa kwenye jambo lolote kwenye maisha yako. Unaweza kupata matokeo unayotaka kwa muda mfupi, lakini hayatadumu kama hujajenga misingi ya uaminifu.

SOMA; Jinsi Ya Kuanzisha Biashara Ikiwa Una Kipato Kidogo.

7. Unahitaji Hekima katika safari yako ya mafanikio. Na hekima inatokana na ujuzi/elimu, uzoefu na ufahamu. Hekima unajijengea mwenyewe kadiri unavyojifunza na kupambana na changamoto za maisha yako. hakuna mtu anayeweza kukupa hekima, hekima unaitengeneza wewe mwenyewe. Hekima itakuwezesha kufanya maamuzi bora katika nyakati za changamoto.

8. Washindi wanazaliwa na washindi wanatengenezwa. Usije ukajiambia kwamba wewe huwezi kuwa mshindi kwa sababu ya maisha uliyopitia, unaweza kujitengeneza na kuwa mshindi kwenye eneo unalotaka. Ili kuwa mshindi ni lazima ujue maana ya mshindi. Mshindi ni mtu ambaye ameonesha uwezo wa juu kwenye kile ambacho anakifanya. Pia mshindi ni mtu ambaye ananyanyuka tena hata kama hawezi kunyanyuka. Ushindi unaanza na wewe mwenyewe, kwa kuamua kuwa mshindi.

9. Ili uwe mshindi ni lazima ujifunze kutoka kwa washindi wengine. Hivyo kuwa na washindi ambao unawafuatilia kwenye kile wanachofanya. Iwe ni kwenye michezo, biashara kazi na hata maisha. Angalia jinsi washindi wanavyochukulia mambo yao, angalia jinsi wanavyotatua changamoto zao na angalia jinsi wanavyopeleka maisha yao. Kuna mengi sana unayoweza kujifunza kupitia washindi, jifunze na yaweke kwenye maisha yako.

10. Washindi wote wana tabia moja ya kipekee, wanakwenda hatua ya ziada. Washindi siyo watu anaofanya kile wanachoambiwa wafanye na kuishia pale, bali ni watu ambao wanajua kipi kinatakiwa kufanyika wanakifanya halafu wanakwenda mbali zaidi kuhakikisha wanakifanya kwa ubora wa hali ya juu sana. Washindi wanatumia muda mwingi kujiandaa kuliko wengine ambao siyo washindi. Hivi ndivyo watu wanavyoshinda mashindano ya michezo, wanavyopandishwa cheo na wanavyokuza biashara zao, kwa kuwa tayari kwenda hatua ya ziada mara zote.

SOMA; KITABU; MIMI NI MSHINDI, Ahadi Yangu Na Nafsi Yangu.

11. Shindana na wewe mwenyewe ili kuwa bora zaidi. Ni rahisi sana kutaka kuwashinda wengine, kwa sababu unaweza kujilinganisha nao kwa nje lakini kumbuka hakuna anayefanana na wewe kwa kila kitu. Hivyo unaweza kuwashinda wengine, lakini ukawa bado hujashinda, kwa sababu unaweza kuwa hujafikia uwezo mkubwa uliopo ndani yako. mara zote shindana na wewe mwenyewe. Hatua yoyote unayopiga kwenye maisha yako jiulize je hiki ndiyo bora kabisa ninachoweza kufanya? Jibu linatakiwa kuwa hapana halafu uongeze ubora zaidi. Ukijilinganisha na wewe unaweza kujiona umeshakuwa bora kumbe unajilinganisha na watu wenye uwezo mdogo sana ukilinganisha na ulionao wewe.

12. Hakuna njia yoyote ambayo imenyooka moja kwa moja, hakuna mpango wowote ambao unakwenda kama ulivyopangwa kwa asilimia 100. Hivyo kuwa na mipango mizuri lakini pia kuwa tayari kubadilika pale mambo yanapokwenda tofauti na ulivyotegemea. Hivi ndivyo washindi wanavyoweza kuzivuka changamoto wanazokutana nazo na kushinda. Usiwe mgumu kubadilika, kuwa tayari kubadilika kadiri mazingira yanavyobadilika.

13. Biashara ni kitu kimoja, KUTATUA MATATIZO YA WATU. Kama unataka kuwa kwenye biashara na ufanikiwe, basi tafuta matatizo yanayowasumbua watu na yatatue. Angalia ni kipi ambacho watu wanasumbuka nacho a waletee suluhisho. Ukifikiria kutatua matatizo ya watu, mara zote utaziona fursa za kuanzisha na kukuza biashara yako.

14. Hakuna mtu yeyote ambaye amepata kitu chochote kiurahisi. Hivi ndivyo tunavyopenda kuwaona washindi, kama watu fulani ambao wamebahatika kufika kwenye ushindi. Tunawaona pale ambapo wameshashinda, lakini hatuwaoni wakati wanajiandaa kushinda. Wanajiandaa kwa mateso makubwa, wanaweka juhudi kubwa kuliko ambavyo wengine wapo tayari kuweka, na hili linawafanya washinde. Kama unataka kuwa mshindi, ni lazima ujitoe, uache kujionea huruma na uweke juhudi kubwa mno.

SOMA; KITABU; KWA NINI MPAKA SASA WEWE NI SIO TAJIRI.

15. Njia bora kabisa ya kutatua matatizo au changamoto, ni kujiandaa kabla tatizo lenyewe halijatokea. Hakuna kitu kinachoumiza kama kukutana na tatizo ambalo hukuwa umejiandaa, washindi hawafanyi hivyo. Mara zote wanajiandaa. Na wanajiandaa kwa kujiuliza swali hili muhimu sana; JE NI TATIZO GANI LINAWEZA KUJITOKEZA? Jiulize swali hili kwenye kila unachofanya na fanyia kazi yale majibu unayoyapata. Hakikisha unakuwa na uelewa wa kila namna inayoweza kwenda tofauti na ulivyopanga na ni hatua zipi utakazochukua.

16. Weka umakini na mawazo yako yote kwenye kile kitu unachokifanya, kwa wakati husika. Washindi wote wanaweka mawazo yao kwenye kile wanachofanya na hivyo kulazimisha akili zao kuja na mawazo bora ya ushindi. Lakini wanaoshindwa wanatawanya mawazo yao kwenye mambo mengi na hivyo kushindwa kutumia akili zao vizuri. Chochote unachochagua kufanya, weka umakini na mawazo yako yote pale, utashangaa jinsi akili yako inavyoweza kukuletea matokeo bora.

17. Jitengenezee mwendo kasi wa mafanikio, kufanikiwa kwenye jambo moja haimaanishi utaweza kufanikiwa kwenye kila kitu. Unachohitaji ni kuwa na mwendokasi wa mafanikio ambao utakuwezesha kuendea kila changamoto kwa hamasa kubwa. Unaweza kujitengenezea mwendokasi wako kwa kujua jinsi mwili wako unavyofanya kazi. Jua ni wakati gani unakuwa na ubunifu mkubwa na nguvu kubwa za kufanya kazi. Wengine wako vizuri wakati wa asubuhi, wengine wakati wa jioni. Jua muda mzuri kwako na utumie vizuri.

18. Matatizo, vikwazo, makosa na hasara ni sehemu ya maisha. Ni vitu ambavyo tunatakiwa kuvikubali ili maisha yaweze kwenda. Hatupaswi kurudishwa nyuma na mambo haya badala yake yanahitaji kutusukuma kuelekea kwenye ushindi zaidi. Jifunze kwa kila unalopitia, ili usirudie kufanya kosa moja mara mbili.

SOMA; Barua Ya Wazi Kwa Wahitimu Wa Elimu Ya Juu Mwaka 2016, Ukweli Ambao Umekuwa Unafichwa Kwa Miaka 20 Iliyopita.

19. Mara nyingi watu watakuwa wanafurahia kukudharau na kudharau mafanikio yako, usikubali watu hawa wakurudishe nyuma, badala yake jikubali wewe mwenyewe, jua kile ambacho unataka na kifanyie kazi. Jua ya kwamba ndani yako una uwezo mkubwa na usisite kusema mbele ya watu kuhusu wewe na kile unachofanya. Hii ndiyo njia ambayo watu watakujua na kujua kile unachofanya, na pia kuwashinda wale wanaokudharau.

20. Wakati mambo yanakwenda hovyo, wakati kila mtu anapitia changamoto ndiyo wakati ambao wengi wanafanya mabadiliko makubwa. uhitaji unawalazimisha watu kuwa wabunifu. Mara zote tumia wakati mgumu unaopitia kuhakikisha unafanya mabadiliko makubwa pale unapopitia wakati mgumu. Kwa sababu huu ndiyo wakati ambao utalazimika kubadilika hivyo badilika na kuwa bora zaidi. Mara zote kuwa na mpango mbadala, usiwe na mpango mmoja pekee, unapokuwa kwenye changamoto ni wakati wa kuangalia mpango mwingine unaoweza kukufikisha kwenye ndoto zako.

Kuna mambo mengi sana kuhusu biashara na maisha tunayoweza kujifunza kupitia Donald Trump, katika kujiandaa kwa maisha ya ushindi na mafanikio.

Fanyia kazi haya ambayo umejifunza kwenye uchambuzi wa kitabu hiki ili uweze kuona matokeo bora kwenye maisha yako.

Kupata vitabu vya Kiswahili vya kujisomea ili kuweza kufanikiwa kwenye kazi, biashara na maisha kwa ujumla, tembelea MOBILE UNIVERSITY (www.mobileuniversity.ac.tz)
Rafiki na Kocha wako,
Makirita Amani,
www.kisimachamaarifa.co.tz/makirita

KUHUSU AMKA MTANZANIA

AMKA MTANZANIA ni mtandao unaokuhamasisha wewe mtanzania kuchukua hatua juu ya maisha yako. Kupitia mtandao huu utajifunza na kuhamasika ili uweze kuchukua hatua ya kufikia mafanikio makubwa. Kama unataka kutumiwa makala nzuri na vitabu moja kwa moja kwenye email yako, BONYEZA MAANDISHI HAYA na ujaze fomu. KARIBU SANA UJIFUNZE NA KUHAMASIKA

Pata Makala Inapotoka

Weka email yako hapa na uwe wa kwanza kupata makala nzuri inapowekwa kwenye mtandao huu.

Washirikishe Wengine Makala Hii Nzuri

Makala Zinazohusiana na Hii

2 comments:

USIACHE KUWEKA MAONI YAKO HAPA.

© 2013 AMKA MTANZANIA. WP Theme-junkie converted by BloggerTheme9
Blogger templates | Distributed By: BloggerBulk Proudly Powered by Blogger.
back to top