MUHIMU KUSOMA;

Vitu Viwili Unavyopaswa Kuwekeza Ili Kuweza Kutengeneza Kipato Kwenye Intaneti.

Habari rafiki? Sheria ya asili inasema kila mtu anavuna kile alichopanda, na hiyo ipo wazi kwenye kila jambo tunalofan...

Thursday, December 31, 2015

Mambo Matano(5) Muhimu Ya Kujifunza Kwenye Kurasa 365 Za Mwaka 2015 Na Mazuri Yanayokuja 2016.

Posted by Makirita Amani  |  at  Thursday, December 31, 2015 No comments

Habari za wakati huu rafiki yangu?
Naamini uko vizuri sana na unaendelea vyema na mipango yako ya kuboresha maisha yako.
Leo nimeandika ukurasa wa 365 katika kurasa 365 za mwaka 2015. Kuna mambo mengi nimejifunza kupitia kurasa hizi na nimeona ni vyema na wewe rafiki yangu ukayapata maana yatakusaidia sana.
Mwaka huu 2015 nilianzisha kipengele cha makala kilichoitwa KURASA 365 ZA MWAKA 2015 ambapo lengo lilikuwa kuandika makala moja kila siku kwa siku zote 365 za mwaka huu 2015.
Nimekuwa naandika angalau kila siku kuanzia mwanzoni mwa mwezi Machi mwaka 2013, lakini ni mwaka huu ndio mara ya kwanza kuweza kuandika kila siku kwa mwaka mzima, bila ya kukubali sababu yoyote inizuie, hata kama ilikuwa kubwa kiasi gani.
Kurasa hizi zilianzaje?
Nakumbuka ilikuwa tarehe 01/01/2015, nilikuwa kwenye kivuko mimi pamoja na familia tukielekea kigamboni nilipokea ujumbe kutoka kwa mmoja wa wasomaji wa AMKA MTANZANIA akinitakia heri ya mwaka mpya. Ujumbe ulikuwa unasema, leo ni ukurasa mpya kabisa kwenye kitabu kipya chenye kurasa 365, unaweza kuamua uandike nini kwenye ukurasa huu. Nilipenda ujumbe ule na kuendelea kuutafakari, baadae nikapata wazo kwa nini kila siku nisiwe naamua kuandika kila kurasa ya kitabu hiki ambacho ni mwaka?
Basi siku ile niliporudi nyumbani, japo ilikuwa usiku, nilisema ni lazima nikae chini na kuandika ukurasa huo wa kwanza kabla siku hiyo haijaisha. Niliandika ukurasa huo na nyingine zilizofuata mpaka kufikia leo ukurasa wa 365.
Kwa mwaka mzima nimefanikiwa kuweza kuandika kila siku, na makala hizi nimekuwa naziandika papo kwa hapo inapokwenda hewani na sio kuiandaa muda kabla au siku kadhaa kabla.
Nimekuwa nakutana na siku zenye changamoto lakini sikukubali zizuie mimi kukaa chini na kuandika, hata kama ni maneno machache tu. Kuna siku ambazo ilinibidi kuandika hata usiku ili tu siku isipite sijaandika kurasa ya siku husika.
Mambo muhimu ya wewe kujifunza kupitia makala hizi za kurasa.
1. Unapoona fursa unayoweza kuifanyia kazi usisubiri, anza kuifanyia kazi.
Nakumbuka kauli mbiu yetu kwenye KISIMA CHA MAARIFA mwaka huu ilikuwa JUST DO IT, yaani WEWE FANYA TU. Kama kuna kitu unaona unaweza kukifanya au unahitaji kukifanya, usisubiri mpaka kila kitu kiwe sawa, bali wewe anza kufanya, anza hata kama ni kidogo, utajifunza mengi zaidi wakati unafanya.
2. Fanya kitu kidogo kila siku.
Watu wengi hufikiri mafanikio au ubora ni kitu kinachotokea siku moja. Lakini huo sio ukweli, mafanikio au ubora sio kitu kinachotokea siku moja, bali ni matokeo ya kile unachofanya kila siku. Hivyo kwenye lile eneo ambalo unataka kuwa bora, kwenye lile eneo ambalo unataka kufikia mafanikio makubwa, hakikisha unafanya kitu kila siku, hata kama ni kidogo kiasi gani.
3. Weka sababu yoyote pembeni.
Katika watu karibu wote ambao nimekuwa nawashauri kwa mwaka huu 2015, wana sababu ambazo wanaamini zinawazuia kufikia mafanikio wanayotaka. Wanakuambia, lakini kazi yangu inanibana sana, sina mtaji wa kuanzia, sina ujuzi au uzoefu, nimejaribu nikapata hasara, na sababu nyingine nyingi. Lakini mimi nimekuwa nawaambia kitu kimoja, hebu weka sababu hiyo pembeni, hebu fikiria bila ya kutumia sababu hiyo, na utaona nafasi nyingi sana. Kama ningekuwa nakubali sababu zinizuie nisingeweza kukamilisha kurasa hizi 365 kwa kuandika kurasa moja kila siku.
4. Kuna watu watakubeza, achana nao.
Kuna watu wataona unachofanya sio muhimu, kuna wengine wataona unachofanya ni rahisi sana, hata wao wangeweza kufanya. Watu hawa wala wasikusumbue, kwa kifupi achana nao na endelea kuweka juhudi. Kuna watu wamekuwa wakisema ah kuandika tu, nani anashindwa hivyo. Ni rahisi kuongelea juu, lakini kukaa chini kila siku uandike kwa mwaka mzima sio kazi ndogo. Kuna siku unaweza kuwa hujisikii kabisa kuandika, siku nyingine unafikiri sana lakini hupati cha kushirikisha na mengine mengi. Endelea kukazana kufanya kile unachoamini, kuna wengi atakaokiamini na wengine watakubeza, wewe wafikirie wale wanaoamini unachofanya na achana na wanaobeza.
5. Usitake ukamilifu.
Kama kigezo ingekuwa ni kuwa na ukamilifu basi nafikiri nisingeweza kuandika hata kurasa 100. Makala ambazo nimekuwa naandika kila siku zinatofautiana sana, kuna ambazo hata mwenyewe nikisoma nasema ndio, iko vizuri sana, kuna ambazo nikisoma naona ningeweza kufanya kwa ubora zaidi. Kuna makala nimeandika maneno 100 na, nyingine maneno 500 na. Usikubali kutaka ukamilifu kukuzuie kufanya makubwa, wewe fanya na utaona majibu mazuri.
Nini kinafuata baada ya kurasa hizi 365 za mwaka 2015?
Wakati naanza kuandika kurasa hizi nilikuwa na lengo la kutoa kitabu baada ya kukamilisha kurasa hizi. Lakini siku zilivyozidi kwenda nilianza kuacha yale mawazo ya kitabu, baada ya kuona makala hizi zinatofautiana sana kwa urefu na pia kuna nyingine zinaendana endana. Lakini juzi rafiki yangu na msomaji mwenzetu aliniandikia kwenye kundi letu la wasap kuhusu kutoa kitabu kupitia makala hizi. Hivyo nimerudi kwenye wazo lile la kwanza na nitatoa kitabu cha kurasa hizi 365 za mwaka.
Hivyo kwa kifupi mambo mawili yataendelea kuhusiana na kurasa hizi za makala.
Jambo la kwanza ni kutoa kitabu, ambacho kitakuwa kwenye mfumo wa softcopy, pdf na kama ikiwezekana kitachapwa. Hivyo kuwa tayari kwa kitabu hiko.
Jambo la pili ni kuendelea kwa kurasa hizi, na sasa hazitaitwa tena kurasa 365 za mwaka, bali zitaitwa KURASA ZA MAISHA. Kila siku mpya kwetu ni ukurasa mpya kwenye kitabu chetu cha maisha, na hivyo tunachagua kuandika nini, kwa kile ambacho tunafanya. Lengo langu ni kuweza kuandika kila siku, yaani kila siku mpaka siku ambayo nitaondoka hapa duniani.
Nitajitahidi kadiri ya uwezo wangu kuzishinda changamoto, kutokukubali sababu na kuhakikisha kila siku unapoamka, unakutana na makala mpya ya kurasa ambayo itakuwa mtazamo mpya wa maisha, ili uweze kuishi maisha bora na unayoyafurahia.
Nitakuja na makala nyingine itakayoelezea kurasa hizi za maisha kwa undani zaidi ikiwepo ni pamoja na maeneo ambayo nitakuwa nazingatia sana kwenye uandishi wa kurasa hizo.
Nikushukuru sana wewe rafiki na msomaji wangu ambaye umekuwa ukifuatilia makala hizi za kurasa kila siku. Kwa wale ambao tumeanza pamoja niwashukuru sana na niombe tuendelee kuwa pamoja. Kwa wale ambao mmekuja katikati nawakaribisha sana, kuna mengi mazuri yanayokuja, tuendelee kuwa pamoja pia.
Kama kuna makala yoyote ya kurasa uliikosa fungua hapa na unaweza kusoma makala zote za kurasa.
MUHIMU;
Semina ya 2016 NI MWAKA WANGU imebaki siku mbili za kujiunga, kama unataka kupata nafasi hii ya kuufanya 2016 kuwa mwaka bora sana kwako, soma hapa na uchukue hatua mara moja.
Pia jiunge na KISIMA CHA MAARIFA, humu utapata makala nyingi zaidi pamoja na kuweza kuingia kwenye kundi la wasap ambapo tuna mengi zaidi ya kujifunza na kushirikishana. Kujiunga niandikie ujumbe kwa wasap kwenye namba 0717396253.
Nakutakia kila la kheri katika kuendelea kuyafanya maisha yako kuwa bora zaidi kila siku.
Rafiki na kocha wako,
Makirita Amani,
makirita@kisimachamaarifa.co.tz

Tags:
KUHUSU AMKA MTANZANIA

AMKA MTANZANIA ni mtandao unaokuhamasisha wewe mtanzania kuchukua hatua juu ya maisha yako. Kupitia mtandao huu utajifunza na kuhamasika ili uweze kuchukua hatua ya kufikia mafanikio makubwa. Kama unataka kutumiwa makala nzuri na vitabu moja kwa moja kwenye email yako, BONYEZA MAANDISHI HAYA na ujaze fomu. KARIBU SANA UJIFUNZE NA KUHAMASIKA

Pata Makala Inapotoka

Weka email yako hapa na uwe wa kwanza kupata makala nzuri inapowekwa kwenye mtandao huu.

Washirikishe Wengine Makala Hii Nzuri

Makala Zinazohusiana na Hii

0 comments:

USIACHE KUWEKA MAONI YAKO HAPA.

© 2013 AMKA MTANZANIA. WP Theme-junkie converted by BloggerTheme9
Blogger templates | Distributed By: BloggerBulk Proudly Powered by Blogger.
back to top