MUHIMU KUSOMA;

Vitu Viwili Unavyopaswa Kuwekeza Ili Kuweza Kutengeneza Kipato Kwenye Intaneti.

Habari rafiki? Sheria ya asili inasema kila mtu anavuna kile alichopanda, na hiyo ipo wazi kwenye kila jambo tunalofan...

Tuesday, June 30, 2015

Mambo 20 Niliyojifunza Kwenye Kitabu Kinachoitwa FLIGHT PLAN The Real Secret Of Success.

Posted by Makirita Amani  |  at  Tuesday, June 30, 2015 1 comment

Habari rafiki, ni matumaini yangu waendelea vizuri. Wiki hii tunaendelea na utaratibu wetu wa kushirikishana mambo 20 niliyojifunza kwenye kitabu. Leo tunaangazia kitabu kinachoitwa FLIGHT PLAN The real secret of success. Kitabu kimeandikwa na mwandishi mashuhuri wa vitabu Brian Tracy. Kitabu kinaitwa Flight Plan au kwa Kiswahili Mpango wa ndege au mpango wa kusafiri kwa ndege. Mwandishi anayafananisha maisha na safari, safari ambayo unaweza kutumia usafiri wowote unaotaka, aidha, gari, pikipiki, kwa miguu au ndege. Mwandishi ameandika kitabu hiki ili kumwezesha msafiri achague njia ya kusafiri kwa ndege ili kufika mapema kwenye kusudio lake. Anaelezea kwamba safari ya ndege ndiyo yenye uhakika wa kufika haraka kuliko njia nyingine. Lakini pia anatoa hatua muhimu za kufanya ili uweze kusafiri kwa ndege. Moja wapo ni kujua unakwenda wapi halafu ndiyo uanze kuchagua aina ya ndege uitakayo. Kitabu hiki ni kizuri na cha kipekee pia.
Karibu tujifunze zaidi.
1. Fanya kazi muda wote wa kazi.
Kuanza kazi na kuimaliza ni changamoto kwa watu wengi. Unakuta unafanya kazi fulani, mara umeacha, umeshika kitu kingine, mara umepokea simu, mara umeanza kuchati, halafu ndio unairudia tena ile kazi. Unagusagusa tena hapo, mara unachepuka kwenye mambo mengine, au unaanza kupiga soga za mambo yasiyo ya maana, au una anza kupiga stori mara za michezo mara stori za siasa, halafu siku inaisha. Kama kweli unataka mpango wako uwe kama wa safari ya ndege ni lazima ufanye kazi uimalize ndio ufanye vitu vingine, weka nguvu zako zote kwenye shughuli hiyo. Mfano ndege ikishapaa, hua haina vituo huko angani, ikianza safari ni mpaka imefika kwenye lengo, na rubani wa ndege anakua makini muda wote kufanya marekebisho pale yanapohitajika. Na ndio maana kama ndege umeambiwa itatumia dk 45 toka Uwanja wa KIA kwenda Dar, itatumia dakika hizohizo. Lakini hebu panda daladala uone, au Coaster, unaweza kuchelewa zaidi ya hata saa moja kwa safari za karibu, safari za mbali unaweza kuchelewa hata masaa 3 zaidi ya yale yaliyokua yamepangwa. Jifunze kufanya mpango wako uwe mpango wa ndege ambayo haisimami mpaka imefika kwenye lengo. Work all the time you work.
2. Chagua mustakabali wako (choose your destination). Siri ya hakika ya mafanikio, ni kwamba maisha ni kama safari ndefu ya ndege, lazima kwanza uanze kuchagua unakotaka kufika, halafu uchague ndege na kukata tiketi halafu ndipo uondoke kuelekea kwenye lengo lako. Hauanzi na kuchagua ndege wakati hujui unakwenda wapi. Aina ya ndege utakayopanda itategemea na unakotaka kwenda. Hivyohivyo mpango unategemea lengo. Unapokua na uhakika wewe ni nani, ni nini unataka, na wapi unataka kwenda utakua na mafanikio mara 10 ya mtu wa kawaida ambaye anaamini maisha ndiyo yanaamua yeye apate nini.
3. Fikiri kwa mrengo wa kutoa suluhisho na si kuendeleza tatizo. Watu hodari ni watu wenye kutoa suluhisho zaidi. Wanafikiria suluhisho ni nini, na nini kifanyike, na sio kufikiri tatizo na nani wa kulaumu. Watu hodari Ni watu wenye mtazamo wa mbele zaidi, wakifikiria zaidi ni hatua gani zichukuliwe haraka ili kudhibiti uharibifu au madhara yanayoweza kusababishwa na tatizo lililotokea. Kua hodari leo kwa kuanza kua na mtazamo wa suluhisho kuliko kutafuta nani mchawi anayepaswa kubeba lawama au kuadhibiwa.
4. Chukua hatua ya Kwanza.
Tofauti ya msingi kati ya ukuu (greatness) na ukawaida (mediocrity) ni katika kuchukua hatua ya kwanza. Watu wakuu (great people) wao wanaweka malengo makubwa, wanapangilia hatua zinazotakiwa kufikia kwenye lengo halafu wanachukua hatua ya kwanza. Wanaanza na hatua ya kwanza. Upande mwingine kwa watu wa kawaida, wanakua na matumaini, ndoto, matarajio, na shauku kadhaa, pengine kama vile watu wakuu/waliofanikiwa wanavyokua. Ila sasa Hofu ya kushindwa na kupoteza/hasara inawazidi nguvu wakati wanapotakiwa kufanya maamuzi ili kuchukua hatua ya kwanza, mwishowe wanarudi nyuma.
5. Kama ukifanya vile ambavyo waliofanikiwa wanafanya, ukafanya tena na tena mpaka ikawa tabia yako basi hakuna kitakachoweza kukuzuia wewe kupata matokeo wanayoyapata.
6. Kupata zaidi, lazima uwe zaidi (To have more, you must first be more). Kwa maneno mengine ukitaka kutengeneza maisha tofauti ni lazima uwe mtu wa tofauti kwanza. Lazima ujifunze na kukua na kupata uzoefu muhimu ambao utakupa hekima na ufahamu wa kuishi maisha ya viwango vya juu. Hakuna njia ya mkato
7. Kila mtu anaanzia chini. Kila unayemuona ambaye yuko juu katika tasnia (field) yako kuna wakati walianzia chini kabisa au hata hawakuwepo kabisa kwenye hiyo tasnia. Lakini Leo hii wamefika hapo juu na wanaingiza kipato kikubwa ambacho ni mara kadhaa ya kipato cha mtu wa kawaida. Habari njema ni kwamba vyote ambavyo wengine wamefanya wakafanikiwa hata wewe unaweza kufanya kama tu utaamua kujifunza ni jinsi gani vinafanyika. Hakuna aliye bora kukuzidi na hakuna aliye nadhifu kuliko wewe, walichokuzidi nacho ni kwamba wao walianza mapema kufanya hivyo vilivyowafanya kufikia hapo. Pengine ungeanza na wao ungekua mbali zaidi. There are no limits except those that you impose on yourself with your own thinking.
8. Katika nyanja yeyote uliyochagua itakuchukua miaka 7 kufikia nafasi ya juu. Watu wengi hawapendi kuusikia huu ukweli, lakini huo ndio ukweli, kwamba eneo lolote, liwe biashara, kazi au ufundi, itakuchukua miaka saba ili uweze kufuzu na kubobea katika viwango vya juu kabisa. Itakuchukua miaka saba biashara yako kufikia mafanikio ya juu. Wengi tukisikia hivi tunakata tamaa na kuacha kujiboresha, tukisahau kwamba hata tukiacha muda ndio unakwenda, hata usipofanya chochote hiyo miaka 7 itapita tu, sasa si bora ukafanya kitu ili baadaye ufaidi matunda ya kuutumia muda vizuri. Maana hata usipoutumia muda utakwenda tu.
9. Moja ya tamaa zenye nguvu kwa binadamu ni kutaka kupata kitu bure, au kwa gharama ndogo sana. Hili ni janga kubwa sana, ndio maana watu wengi wanafikiria njia za kufanikiwa haraka haraka na kwa njia rahisi. Na ndio maana unaona wimbi la vijana kwenye michezo kama kamari na mingineyo mwishowe wanaishia mikono mitupu huku hali zao za mwisho zikiwa mbaya kuliko awali. Ukitaka kumshawishi mtu siku za leo mmpe matumaini ya kufanikiwa haraka haraka bila kuvuja jasho. Hata dini nyingi zenye wafuasi wengi siku za leo ni zile zinazowashawishi watu kua watapata mafanikio ya haraka. Hakuna cha bure. No free lunch
SOMA; Naomba Ufanye Changamoto Hii Ya Siku Kumi, Utabadili Sana Maisha Yako.
10. Jiandae kulipa gharama.
Hakuna kirahisi wakati wa kuanza jambo. Kila ufanikishaji mkubwa ni matokeo ya mamia na maelfu ya juhudi ndogo ndogo ambazo hakuna mtu anayeziona au kuzitambua. Kila tajiri unayemuona ni matokeo ya juhudi, ufanyaji kazi kwa bidii na uzoefu wa muda mrefu. Wakati mwingine hata likizo au mapumziko kwao ilikua ni ngumu, kwa maneno mengine walikubali kulipa gharama. Tatizo kubwa linalokumba watu wengi ni kutokutaka kutia bidii ya vitu ambavyo watu wengine hawavioni. Watu wanataka kila wanachofanya waonekane na wapongezwe. Waliofanikiwa ni wale wanaojitoa sadaka (sacrifice) kwenye mambo ambayo ni nadra sana kukuta wakipongezwa maana mambo hayo wengi hawayaelewi.
11. Maboresho yote ya utu wa nje yanaanzia ndani. Ukitaka kua bora nje lazima uanze kujiboresha ndani, maana ulimwengu wako wa nje ni matokeo ya ulimwengu wako wa ndani. Anza kuboresha jinsi unavyowaza, badili imani ulizonazo ambazo si sahihi, badilisha mtazamo wako, badili jinsi unavyofanya maamuzi n.k. Ukiweza kubadilisha ulimwengu wako wa ndani ulimwengu wa nje na huo utabadilika ili kuakisi mabadiliko yaliyotokea ndani.
12. Ubora wa maisha yako ya baadaye utaamuliwa na uchaguzi na maamuzi unayofanya leo, hususani uchaguzi na maamuzi unayofanya katika yale maeneo ambayo ni ya muhimu katika kufanikisha malengo yako na kufikia hatima ya maisha yako. Uchaguzi wa aina ya kazi au aina ya kampuni ya kufanyia kazi, au aina ya biashara utakayoanza, vinaweza kubadilisha kabisa mwelekeo wa maisha yako. Hivyo unapaswa kutumia muda wa kutosha kufikiri na kuridhika kabisa na uchaguzi unaotaka kufanya kabla ya kufanya uamuzi wa mwisho.
13. Msingi wa utajiri ni thamani. Kama lengo lako ni kufanikiwa kifedha, kuna njia moja pekee ya kuweza kupata mafanikio hayo ya kudumu, na njia hiyo ni kuongeza thamani. Mafanikio ya muda mrefu ya utajiri wa kudumu yanatokana nakuongeza thamani katika maisha ya watu. Mafanikio hayo yanatokana na kuwahudumia watu kwa kuwapatia bidhaa na huduma ambazo wanazihitaji na wako tayari kuzilipia ili kuzipata.
14. Unapokua na lengo la kufanikiwa kifedha anza kwa kutengeneza orodha ya njia ambazo utaweza kuzitumia ili kupata matokeo. Jinsi unavyokua na machaguo mengi ndivyo utakavyoweza kufanya maamuzi mazuri zaidi. Kwa Mfano:
· Unaweza kufikia lengo kwa kuanzisha biashara mpya
· Unaweza kununua biashara ambayo ipo inaendelea
· Unaweza kua bora sana kwa kile unachokifanya na kua unalipwa ghali zaidi, na kwa uangalifu ukawa unawekeza na kuweka akiba pesa zako kwa kipindi cha muda mrefu
· Unaweza ukawa unawekeza kwenye mali zisizohamishika (real estate) kama nyumba na ardhi/viwanja, inaweza kua ni kwa kununua nyumba na kuzifanyia ukarabati na maboresho halafu unaziuza kwa bei ya juu zaidi n.k
15. Matumaini sio Mkakati (Hope Is Not a Strategy). Fanya uchunguzi kabla ya kuwekeza muda wako, fedha au hisia zako kwenye kazi, biashara au mahusiano. Usiishie tu kua na matumaini kwamba kila kitu kipo sawa au kitakua sawa. Pata ushauri kwa wale ambao tayari wameshaipita ile njia unayotaka kuipitia na wamefanikiwa. Jifunze kutoka kwa wataalamu, tafuta wale ambao wameshafikia pale unapotaka kwenda uliza wamefikaje hapo. Jifunze na weka mkakati wa kujiboresha zaidi.
16. Uwezo wako wa kufikiri ndio mali yenye thamani zaidi. Thamani ipo katika Uwezo wako wa kufikiri kua wewe ni nani na unataka nini hasa. Zaidi ya asilimia 80 ya mafanikio yako yatakua ni matokeo ya uwezo wako wa kufikiri vizuri na kwa usahihi. Uwezo wako wa kuweka malengo yanayoeleweka, yanayopimika ambayo una shauku kubwa kuyafikia, yenye kuendana na uwezo na vipaji ulivyo navyo, itakua ni hatua kubwa ya kwanza ya wewe kufikia kwenye mustakabli na mafanikio ya maisha marefu. Tunachotakiwa kujifunza ni kutengeneza huo uwezo wa kufikiri, kuweka malengo na kuweza kuyasimamia
17. Fanyika/kuwa mshauri wako mwenyewe (Become Your Own Consultant)
Hebu jaribu kufikiri wewe ni mshauri na umeitwa kuja kumshauri wewe mwenyewe (to advise yourself) kwenye jambo fulani ambalo ni la muhimu wewe kulifanya ili uweze kufikia mustakabali wako. Ukiwa kama mshauri wako mwenyewe, jilazimishe kuwa tulivu, kuwa mpole na uwe na mtazamo chanya katika kupokea ushauri unaojipatia. Jenga tabia hii ya kujishauri mara kwa mara, kabla hujafanya maamuzi yenye athari aidha chanya au hasi kwenye maisha yako kaa chini jipatie ushauri. Hebu piga picha kwamba wewe ndio unamshauri mtu mwingine kwenye hilo jambo, ungetoa ushauri gani, fanya hivyo kwa uhalisia na bila upendeleao wowote. Halafu jitahidi sasa kuupokea ushauri huo hata kama ni mchungu tekeleza. Don’t fall in love with your ideas, especially your initial ideas. Always be open to the possibility that there is a better way to achieve the same goal.
18. Omba/Uliza kile unachotaka. Katika biashara, maisha yako binafsi au kazini, kumbuka vigezo na sheria/taratibu viliwekwa na mtu fulani na vinaweza kubadilishwa na mtu fulani. Hii inaweza kua mshahara, mazingira ya ajira, vigezo vya mkataba wa kazi, gharama za bidhaa au huduma, gharama za kukodisha sehemu ya biashara, vigezo na masharti ya mikopo n.k hivi vyote viliwekwa na watu. Kama haufurahii kitu hapo usiwe mgumu kuuliza/kuomba. Kitu cha tofauti na kilichopangwa. Usiogope jibu la hapana. Kumbuka kabla ya kuomba/kuuliza kitu jibu hua ni hapana. Na kama hata baada ya kuomba jibu limekua hapana, basi ulichopoteza hapo ni hizo sekunde chache tu ulizo tumia kuomba. Ila kama jibu litakua ndiyo, hii inaweza kubadili maisha yako. The Bible says, “You have not because you ask not.” Never be afraid to ask.
SOMA; Kauli Mbili Za Kuacha Kutumia Leo, Maana Zinaashiria Kushindwa.
19. Mali yako isiyoshikika (Your Intangible Assets). Uwezo wako wa kutengeneza kipato (earning ability) ndiyo mali yako hadimu isiyoshikika. Ni vigumu kuikadiria au kuipima. Watu wawili wanaweza kua na akili sawa na wakawa wamepata matokeo sawa wakati wakiwa shuleni, tena inawezekana wamesoma chuo kimoja, na kozi moja, na kuanza kazi pamoja. Miaka kumi baadaye unakuta mmoja wapo amepandishwa cheo mara kadha na anapata kipato mara 5 au 10 zaidi ya mwenzake. Kwanini hii inatokea? Kwa ufupi ni kwamba hawa watu wanatofautiana katika uwezo wao wa kutengeneza kipato (earning ability. Uwezo huo unaweza kuwa unaongezeka thamani au unashuka thamani. Unapoweka juhudi za kudumu katika kujifunza, kuendelea kuongeza maarifa na ujuzi ili kuongeza thamani popote pale unapokua, uwezo wako wa kuingiza kipato unaongeza thamani yake. Kwa maneno mengine ni kwamba lazima kipato chako lazima kiongezeke.
20. Tengeneza mpango mbadala (Plan B). Endapo mpango wako wa kwanza utashindwa kufanya kazi, kusonga kwako mbele kwa haraka kutategemea mpango mbadala au Plan B. Kamwe usidhanie (assume) kila kitu kitaenda sawia kama kilivyo kwenye mpango wa kwanza. Kama upo bado shuleni, kama Plan A ni kuajiriwa, basi weka na Plan B, ili ukifika mtaani, ajira ikishindikana uwe una chakufanya yaani hiyo Plan B. Changamoto ni kwamba hata hiyo Paln A wengi hawana, ndiyo maana Plan B nayo inakua ngumu. Unakutana na mtu kamaliza chuo mwaka umeisha hana ajira, ukimuuliza unafanya nini sasa, anasema anasubiria bado serikali haijatoa nafasi za ajira, au mwingine anaporomosha malalamiko lukuki kwa serikali ilivyoshindwa kutoa ajira kwake na wenzake. Ukiona mtu wa namna hiyo ujue kakosa Plan B. Always develop a “Plan B” in case your first plan doesn’t work out. Never assume that everything will turn out the way you expect
Asanteni sana
Tukutane wiki ijayo
Makala hii imeandikwa na Ndugu Daudi Mwakalinga mwandishi, mhamasishaji na mshauri katika masuala ya kilimo. Unaweza kuwasiliana naye kwa simu 0763 071007 au barua pepe daudimwakalinga@yahoo.com au dd.mwakalinga@gmail.com

KUHUSU AMKA MTANZANIA

AMKA MTANZANIA ni mtandao unaokuhamasisha wewe mtanzania kuchukua hatua juu ya maisha yako. Kupitia mtandao huu utajifunza na kuhamasika ili uweze kuchukua hatua ya kufikia mafanikio makubwa. Kama unataka kutumiwa makala nzuri na vitabu moja kwa moja kwenye email yako, BONYEZA MAANDISHI HAYA na ujaze fomu. KARIBU SANA UJIFUNZE NA KUHAMASIKA

Pata Makala Inapotoka

Weka email yako hapa na uwe wa kwanza kupata makala nzuri inapowekwa kwenye mtandao huu.

Washirikishe Wengine Makala Hii Nzuri

Makala Zinazohusiana na Hii

1 comments:

USIACHE KUWEKA MAONI YAKO HAPA.

© 2013 AMKA MTANZANIA. WP Theme-junkie converted by BloggerTheme9
Blogger templates | Distributed By: BloggerBulk Proudly Powered by Blogger.
back to top