MUHIMU KUSOMA;

Vitu Viwili Unavyopaswa Kuwekeza Ili Kuweza Kutengeneza Kipato Kwenye Intaneti.

Habari rafiki? Sheria ya asili inasema kila mtu anavuna kile alichopanda, na hiyo ipo wazi kwenye kila jambo tunalofan...

Thursday, February 19, 2015

Makosa 6 Unayofanya Wakati Unapotaka Kubadili Tabia, Zinazokuzuia Kwenye Mafanikio.

Posted by Imani Ngwangwalu  |  at  Thursday, February 19, 2015 No comments

Mara nyingi tabia tulizonazo zinauwezo wa kutufanya tukafanikiwa ama tukashindwa kufikia mafanikio makubwa katika maisha yetu. Kama ambavyo tumekuwa tukizungumza mara kwa mara katika mtandao huu wa AMKA MTANZANIA na KISIMA CHA MAARIFA kwamba, ili kuwa na mafanikio makubwa unayoyahitaji, ni muhimu kwako  kujenga tabia za mafanikio zitakazokuwezesha kufikia mafanikio hayo kwa urahisi.

Kwa kujua umuhimu wa tabia za mafanikio katika maisha yako, inawezekana kwa namna moja ama nyingine umejaribu kubadili tabia zako mbaya zinazokuzuia kwenye mafanikio, lakini kwa bahati mbaya umekuwa ukishindwa mara kwa mara. Kushindwa huku kumekuwa hakuji kwako kwa bahati mbaya kama unavyofikiri,  ila kunatokana na makosa ambayo umekuwa ukiyafanya mara kwa mara wakati unataka kubadili tabia zako. 

Kwa kufanya makosa hayo bila kujua yamekuwa yakikupelekea  wewe kushindwa mara kwa mara kubadili tabia zako mbaya. Ni jambo ambalo limekuwa likikuuma, ukizingatia unayahitaji mafanikio katika maisha yako. Huna haja ya kuumia, kusononeka ama kukata tamaa nakuona maisha basi tena kwako. Badili mwelekeo wako na acha kufanya makosa haya, ambayo yamekuwa yakikugharimu kila unapotaka kubadili tabia zako mbaya zinazokuzuia kwenye mafanikio. Unajua ni makosa gani?

Haya Ndiyo Makosa 6 Unayofanya Wakati Unapotaka Kubadili Tabia,  Zinazokuzuia Kwenye Mafanikio.

 1. Kujaribu kubadili tabia nyingi kwa wakati mmoja.
Hili moja ya kosa kubwa ambalo umekuwa ukilifanya wakati unapojaribu kubadili tabia zinazokurudisha nyuma kimafanikio. Inawezekana ukawa unatabia nyingi zinazokuzuia kwenye mafanikio kama kutokujisomea, kupoteza muda sana, kuwa na matumizi mabaya ya pesa na hata kuwa mtu wa kulaumu bila kuchukua hatua juu ya maisha yako. 

Unapotaka kubadili tabia kama hizi kwa pamoja kuna wakati unaweza ukajikuta unashindwa. Hivyo, ili kufanikiwa ni vizuri ukang’ang’ania kubadili tabia moja kikamilifu kwanza, halafu wakati unaendelea kubadili hizo zingine kidogo kidogo. Hili ni kosa ambalo wengi wamekuwa wakilifanya na kosa hili limepelekea wengi kukata tamaa na kuhisi ni vigumu tabia hizi kubadilika, kitu ambacho sio kweli.

 

2. Umekuwa ukikata tamaa mapema pale unaposhindwa.
Tunapoongelea zoezi la kujenga tabia za mafanikio. Huwa ni zoezi ambalo linahitaji uvumilivu na kuna wakati ikilazimika kujitoa mhanga kabisa ili kuleta matokeo chanya unayoyahitaji. Wengi huwa wanajikuta ni watu wa kushindwa kubadili tabia zao kutokana na kushindwa kwao mara moja na hulazimika kususa na kuona basi haiwezekani tena kwao kufanikiwa. Unaposhindwa kumbuka sio mwisho wa safari, acha kukata tamaa unaposhindwa, jifunze kisha songa mbele hata mambo yako yanapokuwa magumu, mafanikio utayaona.

SOMA; Kabla hujakata tamaa kwa wazo lako kubwa.

3. Umekuwa ukitaka kuona matokeo makubwa tokea mwanzo.
Hili ni kosa kubwa pia ambalo umekuwa ukilifanya wakati unapotaka kubadili tabia zinazokuzuia kuelekea kwenye mafanikio. Watu wengi wenye tabia za kutaka kuona matokeo makubwa tokea wanapoanza mara nyingi huwa ni watu wa kukata tamaa mapema sana. Kwa mfano, kama unatabia  ya matumizi mabaya ya pesa, jiwekee bajeti yako vizuri kisha ifate. Ukiharibu anza upya mapaka matokeo mazuri utayaona tu. Nguvu zako nyingi weka kwenye kubadili tabia, matokeo utayaona kwa muda mwafaka ukifika kwako. Hakuna mabadiliko ya siku moja kama unavyotaka.

SOMA; Kama unashangaa ‘ bigresult now’ hujayaangalia maisha yako vizuri.

4. Umekuwa hutilii mkazo sana mabadiliko unayotaka.
Ni kweli umekuwa una nia ya kubadili tabia zako mbaya zinazokuzuia kwenye mafanikio, lakini kwa bahati mbaya umekuwa huziwekei mkazo mkubwa na kuzingatia kama inavyotakiwa. Kama ni kutaka kubadili tabia ya kusoma, umekuwa ukisoma leo na inapofika kesho unaweza ukaacha na kuendelea na shughuli zingine, tena unakuja kusoma siku nyingine. Kwa mwendo kama huu, kama kweli kama una nia ya kutaka kubadili tabia zako mbaya hautaweza, kwa sababu hii inaonyesha ni kwa jinsi gani hauko makini na mabadiliko ya tabia zako.
5. Umekuwa hujiwekei utaratibu maalum.
Kama kweli unataka kujenga tabia zitakazo kupa mafanikio katika maisha yako, acha tabia ya kutojiwekea utaratibu maalum wa kubadili tabia zako, kama ambavyo umekuwa ukifanya mara kwa mara. Kama unataka kutibu tatizo la matumizi mabovu ya pesa hakikisha una bajeti yako, kama unataka kuamka asubuhi na mapema kila siku, fanya hivyo kila siku bila kukosa pia. Wengi wanakuwa wanashindwa kubadili tabia zao kutokana na kukosa utaratibu maalumu. Jiwekee utaratibu maalum utakaokupa hamasa, kisha uufate na utaona mabadiliko makubwa yanatokea katika maisha yako.

6. Umekuwa huanzi kwa kidogo. 
Ili uweze kubadili tabia zako mbaya zinazokuzuia kufanikiwa ni vyema ukaanza kuzibadili kidogo kidogo, mpaka ukapata matokeo chanya. Kama utataka kubadili ghafla na kupata matokeo ya papo hapo uwe na uhakika nyingi zitakushinda. Kama unataka kujijengea tabia ya kujisomea na kuwa msomaji mzuri. Huhitaji kumaliza kitabu chote kwa siku moja ama kusoma kurasa nyingi sana. Unachotakiwa kufanya ni kusoma kurasa chache kila siku. Halafu utakuwa unaongeza kurasa zaidi siku hadi siku. Anza kufanya mabadiliko kidogo kidogo juu ya tabia zinazokuzuia kufanikiwa na mwisho utaona mabadiliko makubwa.
Kumbuka, tabia zetu ndizo zinazotengeneza ama kubomoa maisha yetu kwa sehemu kubwa sana. Uwezo wa kubadili tabia zako mbaya zinazokuzuia kwenye mafanikio unao. Utapata kila unachokihitaji katika maisha yako kama utaepuka makosa hayo yanayokuzuia kuwa na tabia bora za mafanikio. Unahitaji kuchukua hatua zaidi kwa kujiamini na kisha kusonga mbele. Kila kitu kinawezekana.

Nakutakia kila la kheri katika safari yako ya mafanikio iwe ya ushindi. Kwa kupata maarifa zaidi juu ya TABIA ZA MAFANIKIO hakikisha unajiunga na KISIMA CHA MAARIFA leo kwa kuboresha maisha yako.

Kwa makala nyingine nzuri hakikisha unatembelea DIRA YA MAFANIKIO kujifunza na kuhamasika kila siku, mpaka maisha yako yaimarike.
IMANI NGWANGWALU,


KUHUSU AMKA MTANZANIA

AMKA MTANZANIA ni mtandao unaokuhamasisha wewe mtanzania kuchukua hatua juu ya maisha yako. Kupitia mtandao huu utajifunza na kuhamasika ili uweze kuchukua hatua ya kufikia mafanikio makubwa. Kama unataka kutumiwa makala nzuri na vitabu moja kwa moja kwenye email yako, BONYEZA MAANDISHI HAYA na ujaze fomu. KARIBU SANA UJIFUNZE NA KUHAMASIKA

Pata Makala Inapotoka

Weka email yako hapa na uwe wa kwanza kupata makala nzuri inapowekwa kwenye mtandao huu.

Washirikishe Wengine Makala Hii Nzuri

Makala Zinazohusiana na Hii

0 comments:

USIACHE KUWEKA MAONI YAKO HAPA.

© 2013 AMKA MTANZANIA. WP Theme-junkie converted by BloggerTheme9
Blogger templates | Distributed By: BloggerBulk Proudly Powered by Blogger.
back to top