MUHIMU KUSOMA;

Vitu Viwili Unavyopaswa Kuwekeza Ili Kuweza Kutengeneza Kipato Kwenye Intaneti.

Habari rafiki? Sheria ya asili inasema kila mtu anavuna kile alichopanda, na hiyo ipo wazi kwenye kila jambo tunalofan...

Thursday, June 5, 2014

Mambo 12 Unayotakiwa Kuanza Kuyafanya Katika Maisha Yako

Posted by Makirita Amani  |  at  Thursday, June 05, 2014 No comments

NA IMANI NGWANGWALU, TANGA TANZANIA

Ili kujenga mafanikio ya kudumu kuna mambo ambayo katika maisha inatakiwa tufanye na mengine kutofanya kabisa. Tutatimiza ndoto zetu tu kama tutafanya mambo fulani katika maisha yetu mara kwa mara. Ni wakati muafaka wa wewe kuelekeza nguvu na muda wako kufanya mambo ambayo yataleta mabadiliko makubwa katika maisha yako leo na kesho.

Usipoteze muda wako kufanya vitu ambavyo havikusaidii. Muda unao mchache sana huwezi kufanya kila kitu ukiwa hapa Duniani. Kama utajikuta wewe unang’ang’ania kutaka kufanya kila kitu basi jua maisha yako yatakuwa tupu siku zote. Utakuwa mtu ambaye malengo yako utakuwa unaona hayatimii kwa sababu ya kutaka kufanya kila kitu kinachopita kwenye macho yako. Jifunze kusema NDIO na jifunze kusema HAPANA hata kwa mambo mazuri, fuata malengo yako tu. Unataka kuleta mabadiliko katika maisha yako yapo mambo muhimu kwako ya kufanya ili kusonga mbele.

Yafuatayo ni mambo unayotakiwa kuanza kuyafanya katika maisha yako ambayo yatabadili mtazamo wako na maisha yako kwa ujumla:-

1. Anza kujifunza kuisikiliza sauti ya ndani mwako.

Ni kitu muhimu sana kujifunza kuisikiliza sauti inayotoka ndani mwako. Katika maisha yetu zipo sauti nyingi sana tunazozikiliza lakini wengi wetu tunashindwa kujisikiliza wenyewe. Unapofanya jambo lolote au maamuzi yoyote kwanza hakikisha umeisikiliza sauti ya ndani mwako inasema nini. Unaweza ukapewa ushauri wa jambo fulani au wazo zuri la kufanya katika biashara lakini kabla ya kutekeleza ni muhimu kuisikiliza sauti ya ndani inasemaje? Sauti ya ndani ni wewe mwenyewe, usipojisikiliza wewe mwenyewe maisha yako yatakuwa ya kujuta na kujilaumu kwamba ningejua.Fanya kile ambacho sauti yako ya ndani inasema ufanye achana na kelele za nje katika maisha hizo zipo tu na wala hazitakuja kuisha.

image

2. Anza kufanyia kazi ndoto zako kila siku.

Hakuna kulala, hakuna kusubiri fanyia kazi malengo yako. Hata uwe na malengo makubwa vipi, fanya kitu kidogo juu ya malengo yako hayo na usisubiri kesho. Ukifanyia kazi malengo yako hata kama ni kwa kidogo utajikuta unasogea na ipo siku utashangaa umeyatiza malengo kuliko ungekaa na kusubiri ufanye kesho au siku nyingine. Safari yoyote ndefu huwa inaanza kwa hatua moja hata iwe ndefu vipi na malengo yako hivyo hivyo. Usiache kufanya kitu katika malengo yako fanya kitu kila siku.

3. Anza kujifunza kutokana na makosa.

Wengi wetu huwa hatujifunzi kutokana na makosa zaidi ya kuumia na kulaumu. Kama unataka maisha yako yawe safi bila makosa huwezi fanikiwa sana. Kila binadamu kwa sehemu yake anakosea kwa hiyo huna haja ya kuogopa makosa. Makosa ni chachu ya maendeleo yanatufundisha tuwe makini zaidi na tuongeze juhudi.Pia makosa ni moja kati ya hatua muhimu sana ya maendeleo. Acha kuogopa makosa bali jifunze kutokana na makosa pengine uliyofanya halafu chukua uzoefu na songa mbele.

4. Anza kuweka nguvu ya ushindani ndani mwako.

Mtu pekee ambaye unaweza ukashindana nae ni wewe mwenyewe na si vinginevyo. Katika maisha yako usijaribu kushindana na mtu mwingine zaidi yako.Kama utakuwa mtu wa kushindana na wengine hutafika mbali utakatishwa tamaa tu na unaoshindana nao. Jukumu kubwa ulilonalo ni kujitahidi wewe mwenyewe kuwa bora zaidi ya jana. Nguvu zako zote elekeza katika kushindana na ‘rekodi’ zako zote ambazo umewahi kuziweka katika maisha yako. Kushindana na wengine nje ya wewe ni kupoteza muda na nguvu kwani kila mtu ana malengo yake na njia zake.

5. Anzisha mahusiano na watu chanya.

Hakikisha unazungukwa na watu ambao wana mitazamo chanya katika maisha yako. Kama ni marafiki usiwe na marafiki tu kuwa na marafiki wanaokujenga. Hauwezi ukawa kila kitu kwa kila mtu ila unaweza unaweza ukawa kila kitu kwa watu wachache tu. Chagua watu muhimu katika maisha yako watakaokufanya ufanikiwe na sio kukurudisha nyuma. Ni bora kuwa na watu wachache ambao ni chanya kuliko kuwa na watu wengi ambao ni hasi.

6. Anza kutumia muda wako vizuri

Usipoteze muda wako kwa namna yoyote ile. Jifunze sasa kutumia muda wako vizuri na usipoteze hata dakika. Kumbuka watu wenye mafanikio zaidi Duniani ni wale ambao wamemudu kutumia muda wao vizuri. Ukimudu kutumia muda wako vizuri utafika mbali sana.

7. Anza kutumia vipaji ulivyo navyo kukufanikisha zaidi.

Watu wengi hawajui namna ya kutumia vipaji vilivyomo ndani mwao. Kama unataka maisha yako yawe ya mafanikio zaidi kuza na tumia vipaji vyako. Kipaji chako kinapotumika kinatoa matokeo makubwa sana (Unaweza ukasoma pia jinsi ya kugundua vipaji vilivyopo ndani yako)

8. Anza kujifunza kuishi sasa.

Jenga tabia ya kufurahia maisha yako kwa uzuri wake. Usibebe mizigo mingi ndani ya siku moja. Furahia maisha kwa kuishi leo. Acha kufikiria sana mambo ya jana ambayo pengine yalikuumiza hayo yameshapita maisha yanaendelea tena. Ukiweza kumudu kuishi leo maisha yatakuwa ya furaha na amani kwako.

9. Anza kujifunza kukabiliana na changamoto.

Watu wengi linapokuja suala la changamoto huwa wanakwepa kwa namna moja au nyingine.Wapo ambao hujikuta wameishia baa kwa kupoteza mawazo jambo ambalo ni ukwepaji wa changamoto pia. Pambana na changamoto zako maisha utayaona kwa mtazamo tofauti.

10. Anza kujifunza kujisamehe wewe mwenyewe

Kama kuna sehemu umekosea kwenye maisha yako na unaumia kutokana na makosa uliyofanya huna haja ya kuendelea kuumia sana jisamehe mwenyewe. Kila mtu anakosea na makosa ni sehemu ya maisha.

11. Anza kujifunza kusaidia watu.

Usikae mbali sana na jamii yako. Linapokuja suala la kutoa msaada toa kama uwezekano upo. Watu wengi wenye mafanikio makubwa Duniani hawako mbali sana na jamii zao ni watu wa kujali na kutoa misaada.

kitabu kava tangazo

12. Anza kujifunza kufurahia mafanikio uliyo nayo.

Kama umefanikiwa jambo kwa sehemu ni vizuri ukalifurahia.Usingoje hadi uwe na mafanikio makubwa sana.Hii itakusaidia kukupa nguvu na hamasa ya kusonga mbele zaidi.

Kuna vitu vingi ambavyo ili tuweze kubadili maisha yetu ni lazima tuvifanye hivyo ni baadhi tu vinaweza vikawa msaada kwako kwa namna moja au nyingine nakutakia mafanikio mema.

UNAWEZA KUWASILIANA NA MWANDISHI WA MAKALA HII IMANI NGWANGWALU KWA 0767048035.

KAMA NA WEWE UNA MAKALA NZURI ULIYOANDIKA NA UNAFIKIRI INAWEZA KUWAAMSHA WATANZANIA TAFADHALI NITUMIE KWENYE amakirita@gmail.com

MAKALA ISIWE IMEWEKWA KWENYE BLOG AU CHOMBO KINGINE CHA HABARI, IWE IMETUMIA KISHWAHILI RAHISI NA KINACHOELEWEKA NA IWE NA MANENO KATI YA 500 NA 1000 KARIBU SANA.

Tags:
KUHUSU AMKA MTANZANIA

AMKA MTANZANIA ni mtandao unaokuhamasisha wewe mtanzania kuchukua hatua juu ya maisha yako. Kupitia mtandao huu utajifunza na kuhamasika ili uweze kuchukua hatua ya kufikia mafanikio makubwa. Kama unataka kutumiwa makala nzuri na vitabu moja kwa moja kwenye email yako, BONYEZA MAANDISHI HAYA na ujaze fomu. KARIBU SANA UJIFUNZE NA KUHAMASIKA

Pata Makala Inapotoka

Weka email yako hapa na uwe wa kwanza kupata makala nzuri inapowekwa kwenye mtandao huu.

Washirikishe Wengine Makala Hii Nzuri

Makala Zinazohusiana na Hii

0 comments:

USIACHE KUWEKA MAONI YAKO HAPA.

© 2013 AMKA MTANZANIA. WP Theme-junkie converted by BloggerTheme9
Blogger templates | Distributed By: BloggerBulk Proudly Powered by Blogger.
back to top