MUHIMU KUSOMA;

SEMINA; Elimu Ya Msingi Ya Fedha (Basic Financial Education).

Habari za leo rafiki yangu, Mwanzoni mwa mwaka huu 2017 niliendesha semina yetu ya kwanza ya mwaka 2017 kwa njia ya mtandao. Na nilikua...

Wednesday, May 21, 2014

Hizi Ndio Aina Tano Za Dharura Za Kifedha(Angalizo; Michango Ya Sherehe Sio Mojawapo)

Posted by Makirita Amani  |  at  Wednesday, May 21, 2014 1 comment

Naomba nikiri kwamba mimi ni muumini mzuri wa sheria ya kujilipa mimi mwenyewe. Kwa kipato chochote ninachopata asilimia kumi najilipa mimi mwenyewe kama ninavyolipia huduma na bidhaa nyingine. Na nikishajilipa kiwango hicho nasahau kabisa kama kipo hivyo inapotokea hitaji la fedha zaidi sikimbilii akiba ya fedha niliyojilipa mwenyewe bali kutafuta njia nyingine ya kupata fedha hiyo ya ziada.

Nimekuwa nikishauri watu na kuandika sana juu ya umuhimu wa kujilipa katika kila sehemu ya mapato yako. Kwenye makala unawalipa watu wote kasoro huyu mmoja wa muhimu nilieleza jinsi unavyoweza kutekeleza ushauri huu hata kama una kipato kidogo. Kama hukuisoma bonyeza hayo maandishi kuisoma.

Kuna watu wengi wanafuata ushauri huu na wamekuwa wakinijulisha ni jinsi gani umekuwa ushauri mzuri kwao. Ila ukiendelea kuwafuatilia na kutaka kujua wamefikia kiwango gani kuna baadhi wanakuwa wamerudi nyuma. Mtu anakuambia nilikuwa naendelea vizuri lakini ikatokea dharura ambayo ilinilazimu kutumia fedha yote.

Yawezekana na wewe ni mmoja wa watu ambao unateseka na dhana hii ya kujiwekea akiba. Kila ukiweka kabla hujafanya jambo la maana inatokea dharura na unajikuta umetumia akiba yote.

VINJA KIBUBU

Leo nataka tujadili dharura za kifedha ili tuweze kusaidiana kupunguza matumizi yasiyo ya msingi kwenye akiba zetu. Matumizi ya pesa kwa kisingizio cha dharura inaweza isiwe dharura kweli na ikawa ni sehemu ya kutumia fedha bila mipango mizuri.

Kabla hatujaziona dharura zitakazokulazimu kutumia akiba yako kwanza tuangalie kwa undani umuhimu na matumizi ya hii akiba.

Akiba unayojiwekea kwa kujilipa asilimia 10 ya mapato yako sio akiba unayoweza kuitumia kirahisi tu. Kwanza jua ile fedha sio yako na ni kama haipo kwa sababu kuna mtu umemlipa. Kwani unavyonunua nguo kwa fedha yako kuna siku unairudisha na kupewa fedha hiyo? Hakuna kitu kama hiko, hivyo hii asilimia kumi umejilipa wewe kama unavyowalipa wauza nguo, wauza vyakula, na watoa huduma mbalimbali.

Shughuli nyingine za maendeleo ni lazima uwe na akiba nazo ili kuweza kuenda vizuri, ila ile asilimia 10 isahau kabisa.

Ila inapotokea dharura kubwa ambapo unakuwa umeshatumia akiba zako zote zimeisha hapo ndio unaweza kuingiza mkono kwenye ile asilimia 10. Ili kuepuka uzembe wa kupeleka mkono pale kila mara hapa nakupatia dharura tano za kifedha ambazo zinastahili kukufanya wewe kuingia kwenye asilimia 10.

Nimeweka angalizo kubwa kwamba michango ya sherehe sio moja ya dharura hizi kwa sababu sehemu kubwa ya watu wanajikuta wanatumia fedha hizo kwenye michango ya aina hiyo.

Tumia fedha yako ya akiba ya asilimia 10 kama tu;

1. Umepoteza kazi au biashara yako.

Kama umefukuzwa au kusimamishwa kazi utahitaji njia ya kukufanya uweze kusimama kiuchumi. Hapa unaweza kutumia akiba yako kutengeneza njia nyingine za kujipatia kipato. Hivyo pia kama umepoteza biashara yako kwa kuingia kwenye hasara kubwa, unaweza kutumia sehemu ya akiba yako hiyo kurudi tena kwenye biashara.

2. Kuna dharura ya kitabibu.

Kama wewe au mtu wa familia yako ana dharura ya kiafya huna budi kutumia sehemu ya akiba yako kusaidia kunusuru afya yako au yake.

3. Una dharura ya sehemu ya malazi.

Kama kuna dharura imetokea nyumbani kwako ambayo itasababisha maisha yawe magumu unaweza kutumia akiba yako kutatua dharura hiyo. Na hapa dharura simaanishi kuifanya nyumba kuwa ya kisasa au kuongeza urembo na kuboresha muonekano bali nazungumzia dharura kama kuna paa linavuja.

4. Una dharura ya kusafiri au umepata msiba.

Kama inakubidi usafiri na ni lazima sana kwa shughuli zako au maisha yako hapo unaweza kutumia fedha ya akiba. Kama umepata msiba wa kifamilia au ndugu wa karibu katika wakati ambao haupo vizuri kifedha unaweza kutumia akiba yako kukamilisha safari ya kumpumzisha ndugu yako. Ila kuwa makini sana usitumie kivuli hicho kutumia fedha ambapo sio kwa lazima.

5. Dharura ya viwezeshaji.

Kama moja ya viwezeshaji muhimu kwenye shughuli zako za kukuingizia kipato kinakosekana unaweza kutumia fedha yako ya akiba. Kwa mfano kama shughuli zako zinategemea sana wewe kuwa na gari halafu ikatokea gari lako limeharibika kwa kiasi kikubwa unaweza kuhitajika kupeleka mkono kwenye akiba yako ili kuokoa jahazi.

Hizo ndio dharura tano tu za kifedha ambazo zitakulazimu kuingia kwenye akiba yako ya asilimia 10. Hivi vitu vingine kama kununua vitu ili kwenda na wakati, michango ya sherehe na anasa nyingine HAZISTAHILI KABISA kupata mchango kutoka kwenye akiba hii muhimu. Kama unahitaji kutoa fedha kwa ajili ya vitu hivyo tafuta kwenye chanzo kingine ila sio kwenye akiba hii muhimu.

Unafikiri kuna dharura nyingine muhimu nimeisahau? Tafadhali nijulishe hapo chini.

Kama unajiuliza kama huwezi kutumia akiba hii kwenye dharura yoyote matumizi yake ni nini? Matumizi ya akiba hii ni kuwekeza ili ikupatie watoto na wajukuu watakaokuwezesha kuwa na uhuru wa kifedha.

TUKO PAMOJA.

kitabu kava tangazo

Tags:
KUHUSU AMKA MTANZANIA

AMKA MTANZANIA ni mtandao unaokuhamasisha wewe mtanzania kuchukua hatua juu ya maisha yako. Kupitia mtandao huu utajifunza na kuhamasika ili uweze kuchukua hatua ya kufikia mafanikio makubwa. Kama unataka kutumiwa makala nzuri na vitabu moja kwa moja kwenye email yako, BONYEZA MAANDISHI HAYA na ujaze fomu. KARIBU SANA UJIFUNZE NA KUHAMASIKA

Pata Makala Inapotoka

Weka email yako hapa na uwe wa kwanza kupata makala nzuri inapowekwa kwenye mtandao huu.

Washirikishe Wengine Makala Hii Nzuri

Makala Zinazohusiana na Hii

1 comments:

USIACHE KUWEKA MAONI YAKO HAPA.

© 2013 AMKA MTANZANIA. WP Theme-junkie converted by BloggerTheme9
Blogger templates | Distributed By: BloggerBulk Proudly Powered by Blogger.
back to top