MUHIMU KUSOMA;

SEMINA; Elimu Ya Msingi Ya Fedha (Basic Financial Education).

Habari za leo rafiki yangu, Mwanzoni mwa mwaka huu 2017 niliendesha semina yetu ya kwanza ya mwaka 2017 kwa njia ya mtandao. Na nilikua...

Wednesday, March 12, 2014

Ukiweza Kushinda Sauti Yako Ya Ndani Hakuna Kitakachokushinda.

Posted by Makirita Amani  |  at  Wednesday, March 12, 2014 No comments

Mara nyingi maadui zetu wakubwa ni sisi wenyewe. Sisi wenyewe tumekuwa wakatishaji tamaa wakubwa kwenye mabadiliko na maendeleo yetu wenyewe. Kwenye jambo lolote kubwa la mabadiliko unalofanya kuna sauti ya ndani yako huwa inakushawishi usifanye.

Kwa mfano unaweza kupanga kuacha tabia fulani ambayo imekuwa inakurudisha nyuma, kwa mfano ulevi. Unaweka mipango kabisa labda unaacha kunywa pombe, baada ya siku mbili au tatu kupita hii sauti inaanza kukushawishi urudi kwenye tabia yako ya zamani. Unaanza kujishauri kwanza nikinywa kidogo sio mbaya, kwanza hata nikinywa sio mwisho wa dunia, watu niliokuwa nakunywa nao watanionaje? Sauti hii inakupa sababu lukuki ambazo zinakufanya urudi kwenye tabia uliyoamua kuacha.

           sauti ya ndani

Wakati mwingine unaweza kuwa umeamua kutengeneza tabia mpya ambayo itayaboresha maisha yako. Kwa mfano tabia ya kuamka asubuhi na mapema kila siku, unaweka mipango mizuri ya kuamka na kutumia muda huo kwa manufaa. Siku ya kwanza unaweza kuamka vizuri kwa sababu ulipania, ila siku zinazofuata sauti iliyoko ndani yako inaanza kukushawishi. “Alarm” inaita unashtuka ila sauti inaanza kukushawishi kwamba sio mbaya kama utaendelea kulala kidogo, hata hivyo dakika tano tu zinakutosha kupumzika kidogo na baadae utaamka. Kama ukisikiliza sauti hii na kusema ulale dakika zingine tano unakuja kuamka masaa mawili baadae.

Sauti iliyo ndani yako imekuzuia kufanya mambo mengi makubwa. Uko hapo ulipo kwa sababu ya kuisikiliza na kuifata sauti yako ya ndani ya kukatisha tamaa. Kama usingekuwa unaisikiliza sauti hii ungekuwa umefanya mambo makubwa sana kwenye maisha yako.

Kumbuka ni mara ngapi umepanga kufanya jambo la kubadili maisha yako ila ukaanza kufikiria hutoweza? Wakati mwingine unafikiria watu watakuchukuliaje, au utaanza kufanya baada ya jambo fulani kutokea. Sababu zote hizi unazokuwa unajipa ili kutofanya jambo sio sababu za ukweli bali ni sauti iliyo ndani yako inaogopa tu mabadiliko.

Hata sababu nyingi za kijinga zinazokuzuia kubadili maisha yako zinatokana na sauti hii ya ndani.(soma; sababu tano za kijinga zinazokurudisha nyuma)

Kwa nini sauti hii ipo?

Sauti hii iliyopo ndani yetu ndio uhalisia wa utu wetu. Kwa asili binadamu hatupendi mabadiliko na pia tuna uvivu mkubwa. Sauti iliyopo ndani yako inakuwa ya kwanza kukukatisha tamaa pale unapofanya jambo linalokuondoa kwenye uvivu au jambo la kubadili maisha yako.

Sauti hii ipo na itaendelea kuwepo, hivyo usihangaike kuiondoa. Kikubwa unachotakiwa kufanya ni kuipuuza.

Kama unataka kufanya mambo makubwa kwenye maisha yako inabidi uweze kuishinda sauti hii ya kukukatisha tamaa inayotoka ndani yako.

kitabu kava tangazo

Tambua unaweza kufanya mambo makubwa kwenye maisha yako kama kweli utaamua kufanya. Pia jua hakuna anayefuatilia sana maisha yako kama unavyohofu kwamba watu watakuchukuliaje, kila mtu anasumbuka na matatizo yake.

Usikubali sauti ya kukatisha tamaa iliyopo ndani yako iendelee kukuzuia kufanya mabadiliko makubwa kwenye maisha yako. Ukiweza kuishinda sauti hii hakuna kinachoweza kukushinda katika safari yako ya mafanikio.

Tags:
KUHUSU AMKA MTANZANIA

AMKA MTANZANIA ni mtandao unaokuhamasisha wewe mtanzania kuchukua hatua juu ya maisha yako. Kupitia mtandao huu utajifunza na kuhamasika ili uweze kuchukua hatua ya kufikia mafanikio makubwa. Kama unataka kutumiwa makala nzuri na vitabu moja kwa moja kwenye email yako, BONYEZA MAANDISHI HAYA na ujaze fomu. KARIBU SANA UJIFUNZE NA KUHAMASIKA

Pata Makala Inapotoka

Weka email yako hapa na uwe wa kwanza kupata makala nzuri inapowekwa kwenye mtandao huu.

Washirikishe Wengine Makala Hii Nzuri

Makala Zinazohusiana na Hii

0 comments:

USIACHE KUWEKA MAONI YAKO HAPA.

© 2013 AMKA MTANZANIA. WP Theme-junkie converted by BloggerTheme9
Blogger templates | Distributed By: BloggerBulk Proudly Powered by Blogger.
back to top