Mara nyingi umekuwa ukifikiria kwa nini maisha yasingekuwa rahisi? Umekuwa ukilalamikia ugumu wa maisha unaotokana na changamoto mbalimbali unazokutana nazo kwenye maisha.
Unaweza kuwa unalalamika sana kuhusu ugumu wa maisha ama changamoto za maisha. Lakini ukifikiri kwa makini hutakiwi kulalamikia ugumu ama changamoto za maisha. Badala yake unatakiwa ufurahie changamoto hizo.
Huelewi kwa nini nasema ufurahie ugumu wa maisha? Endelea kusoma huku ukiyatafakari maisha kwa makini na mwisho utaelewa na kubadili mtazamo wako juu ya ugumu wa maisha.
Umewahi kujiuliza kama kusingekuwa na changamoto maisha yangekuwaje?
Hebu tupate picha kama tungekuwa tunaishi kwenye nchi ya maziwa na asali(kama wengi wetu tunavyoota),
Unalala na kuamka, chakula kipo hakuna haja ya kutafuta. Fedha haina matumizi maana hakuna unachohitajika kununua. Kila unachohitaji kinapatikana bila kutumia nguvu ya ziada!
Kwa picha hiyo maisha yangekuwaje? Unaweza kufikiri yangekuwa maisha ya furaha sana, ila ukitafakari kwa makini yangekuwa maisha mabovu kwa wanadamu kuliko ilivyo sasa.
Kusingekuwa na ugunduzi wowote wa teknolojia, huenda hizi kompyuta tusingezijua kabisa. Nani angejisumbua kugundua vitu vikubwa wakati maisha yanajitosheleza?
Kusingekuwa na burudani unazozifurahia kwa sasa kama filamu, muziki, na michezo mbalimbali. Nani angekuwa tayari kwenda kuumia uwanjani wakati hata akilala anaweza kupata chochote anachotaka?
Kwa ufupi maisha yangekuwa mabovu, yasiyokuwa na furaha na tungeishi kama swala ama simba wanavyoishi porini.
Changamoto za maisha ndizo zimefanya watu wakagundua vitu mbalimbali. Hitaji la kwenda mbali kutafuta mahitaji muhimu lilifanya watu wagundue njia za usafiri. Tatizo la hali ya hewa ya joto sana ama baridi sana lilifanya watu wagundue viyoyozi.
Kwa njia yoyote ile ugumu wa maisha ndio umefanya maisha yakawa bora na yenye furaha.
Sasa kwa nini wewe unataka maisha yawe rahisi? Kwa nini unalalamika maisha ni magumu?
Kulalamikia ugumu wa maisha ni sawa na kutaka tuishi maisha kama ya swala.(soma; tofauti yako na mbuzi ni hii)
Binadamu tuna uwezo mkubwa sana wa kuweza kukabiliana na changamoto yoyote ile tunayokutana nayo. Kulalamikia changamoto ni kuudhalilisha uwezo mkubwa tulio nao.
Acha kulalamikia ugumu wa maisha. Acha kuchukia changamoto za maisha. Furahia kila unapokutana na ugumu ama changamoto kwa sababu hapo ndipo unapoweza kutumia uwezo mkubwa ulioko ndani yako.
Tuzikabili changamoto za maisha ili tuweze kuyafurahia maisha.