Kufanikiwa ni msamiati mpana sana. Pamoja na kuwa na maana kubwa, kila mtu amepanga kufanikiwa na anapenda kufanikiwa. Na ili kufanikiwa kuna vitu vingi sana mtu unatakiwa kufanya.

  Kazi ni njia mojawapo na njia kuu ya kufikia mafanikio yetu kimaisha. Sote tunajua kazi ndio msingi wa maendeleo, hivyo kufanikiwa kwenye kazi ni dalili nzuri kwamba utafanikiwa kwenye maisha.

bored at workhudhuria2

  Kwa kazi yoyote unayofanya, iwe umeajiriwa, umejiajiri ama unafanya biashara, kuna vitu vingi sana unatakiwa kufanya ama kuwa navyo ili uweze kufanikiwa wenye hiyo kazi. Na pia kuna vitu ambavyo ukivifanya ama ukiwa navyo uwezekano wa kufanikiwa unakuwa mdogo sana.

  Hapa utaona dalili kuu nane(8) ambazo kama unazo kuna uwezekano mkubwa upo kwenye njia isiyoelekea kwenye mafanikio. Soma kwa makini uelewe kisha uyatathimini maisha yako, na ufanye maamuzi sahihi kulingana na malengo na mipango ya maisha yako. Unapozisoma dalili hizi jaribu kulinganisha watu unaowafahamu, ambao wanafanya kazi unayofanya na angalia tofauti kati ya waliofanikiwa na ambao hawajafanikiwa.

  Dalili kuu nane(8) za kutofanikiwa kwenye kazi ama shughuli unayofanya.

1. Umekosa hamasa kwa unachofanya. Kama umefikia wakati hakuna kinachokuhamasisha kufanya kazi unayofanya basi uwezekano wa kufanikiwa kwenye kazi hiyo ni mdogo sana ama haupo. Na kama umekosa mapenzi kwenye kazi yako basi hali yako ndio mbaya zaidi.(soma; kama unataka kufanikiwa usifanye kazi)

2. Kila siku asubuhi uko hovyo. Kama kila siku asubuhi unachukia sana kuamka na kuelekea kazini ni dalili kwamba mafanikio kwako yatakuwa magumu. Kama unakuwa mzito kuamka, na unalalamika kukatisha usingizi wako mapema wa ajili ya kwenda kufanya kazi basi kazi unayofanya haikupi hamasa ya kutosha na hivyo itakuwa ngumu sana kwako kufanikiwa.

3. Huwapendi watu unaofanya nao kazi. Kama watu unaofanya nao kazi huwapendi ama hamuendani ni vigumu sana kufanya kazi nzuri na hatimaye kufanikiwa. Na kama humpendi bosi wako pia kazi yako haiwezi kuwa na maana kubwa kwako na hivyo kufanikiwa inakuwa vigumu.

4.  Mara nyingi una msongo wa mawazo na mtazamo hasi juu ya kazi unayofanya. Kama kazi unayofanya inakusababishia msongo wa mawazo au kama una mtizamo hasi juu ya kazi unayofanya ni dalili ya kutofanikiwa kupitia kazi hiyo(soma; msongo wa mawazo, sababu kuu ya matatizo yako)

5. Hakuna jipya unalojifunza. Kama kila siku unafanya kitu kilekile kwa njia zile zile na hakuna vitu vipya unavyojifunza kutokana na kazi unayofanya basi ni vigumu sana kufanikiwa.

6. Matatizo ya kazi zako yanaathiri afya yako na mahusiano yako na familia yako. Kazi zina matatizo mengi, ila kama matatizo yanayotokana na kazi unayofanya yanaadhiri afya yako moja kwa moja ama yanadhiri uhusiano wako na familia yako ni dalili ya kutopata mafanikio makubwa kwa kazi unayoifanya.

7. Huamini unachokifanya ama kampuni unayofanya nayo kazi. Kama huwezi kununua ama kumshauri mtu kununua huduma ama bidhaa inayozalishwa kwenye kazi unayofanya ni dalili ya kutofanikiwa kupitia kazi hiyo. Kama kuna vitu vinakukwaza kiimani ama kiutamaduni kwenye kazi yako pia mafanikio yatakuwa magumu kwako.

8. Hutumii uwezo wako halisi. Kama kazi unayofanya haikuruhusu wewe kutumia uwezo wako halisi, vipaji na ubunifu wako ni vigumu sana kufanikiwa. Pia kama uwezo wako hauthaminiwi kwenye kazi yako ni vigumu sana kufanikiwa.

  Kwa kusoma dalili hizi, yaangalie tena maisha yako ya kazi na kisha ufanye maamuzi sahihi. Kama kweli unataka kufanikiwa ni lazima upende kile unchofanya. Kama una dalili hizi kuna mambo mawili unaweza kufanya, kuacha kazi unayofanya na kutafuta ile unayoipenda, ama kufanya marekebisho kwenye kazi yako na kubadili mtazamo wako juu ya kazi unayofanya.