Una ndoto na malengo makubwa una mipango mizuri sana ila bado hupati mafanikio unayohitaji!
Kila unachofanya unaona hakiwezekani na kujaribu kingine na umekuwa unafanya hivyo mara kwa mara. Kila unapangalia wenzako wanaofanya vitu vingine unaona wao ndio wanafanikiwa ila wewe umekosea kuchagua unachofanya!
Kila siku umekuwa unapanga na kupanga na unataka kuongeza uwezo wako ndio uweze kuanza lakini bado huoni kama unaenda mbele!
Unajikuta njia panda na kuona hakuna unachoweza kufanya na labda una bahati mbaya, wenzako wamefanikiwa kwa sababu unaona wana bahati nzuri.
Unayatafakari maneno ya walikuambia huwezi na kuona walikuwa sahihi.
Kama unakutana na hali hizo usijiumize, hazitokei kwako tu, wengi wamepitia hali kama hizo. Sio kosa lako kuwa kwenye hali kama hiyo.
Umefika kwenye hali hiyo kwa sababu kuna kitu hujakijua ama hujajua umuhimu wake. Wote unaowaona wamefanikiwa walipitia hali kama yako ila kwa kujua hiki utakachojua leo waliweza kusonga mbele na kufikia mafanikio yao.
Hujafanya maamuzi!
Kitu ambacho hujajua ni kwamba HUJAFANYA MAAMUZI, Ndio hujafanya maamuzi.
Unaweza kudhani kuwa na malengo na mipango ni maamuzi ila siyo maamuzi ninayozungumzia hapa. Ni lazima ufanye maamuzi ya kuyasimamia maamuzi yako mpaka utakapofikia maengo yako.
Ni lazima uwe na maamuzi thabiti na yasiyoyumbishwa na mtu yeyote. Ni lazima uwe tayari kuyasimamia maamuzi yako kwa gharama yoyote. Hapo ndipo utakapoweza kuyafikia mafanikio unayotarajia.
Kupanga na kupangua kila siku hakutokufikisha mbali, kila siku utayumbishwa na mwishowe utapotea kabisa na kushindwa kujua unaelekea wapi.
Historia inatufundishwa kwamba watu wote waliokuwa na maamuzi thabiti na kutokubali kuyumbishwa ndio walioweza kufikia malengo yao na ndio walileta mabadiliko makubwa kwenye jamii walizoishi(soma;unajua ulichokuja kufanya duniani?)
Mafanikio yoyote yanatokana na maamuzi thabiti ya kutaka kufikia mafanikio. Fanya maamuzi ya kufikia malengo yako, kisha fanya maamuzi ya kuyasimamia maamuzi yako.