Kuna baadhi ya tabia ama hali ambazo zinawasumbua sana watu. Unakuta mtu anatumia nguvu nyingi kutaka kubadili tabia ama hali fulani aliyonayo. Cha kushangaza ni kwamba tabia ama hali hizo hazitokei tu ghafla, nyingi hutokana na tabia ndogo ndogo zilizofanyika kwa kipindi kirefu mpaka kupelekea kuwa tabia sugu.

  Matatizo mengi yanayowasumbua watu yametokana na tabia zilizoonekana kutokuwa na madhara makubwa ila kwa kurudiwa kwa muda mrefu zinatengeneza matatizo. Tabia nyingi huanza kimzaha mzaha bila ya kufikiri zinaweza kumfikisha wapi mtu.

  Matatizo kama ulevi wa kupindukia, uvutaji, kucheza kamari, utumiaji wa mihadarati, unene, umalaya na hata ukorofi hayakuanza ndani ya siku moja. Matatizo hayo yanatokana na mkusanyiko wa vijitabia vidogo vidogo na mwishowe kuwa tabia sugu.

bad habit

  Kwa tatizo la uzito wa mwili kuzidi(unene) watu tuna tabia ya kula tu bila kuzingatia kanuni za mlo kamili. Mtu anakula chipsi mayai au vyakula vingine vya haraka karibu kila siku. Huwezi kuona madhara ya vyakula hivi ndani ya muda mfupi, ila baada ya muda ndio utaanza kuona kitambi kinatoka na unene usioeleweka. Wakati ukifikiri hio ndio afya, baada ya muda yanakuja magonjwa yanayotokana na tabia hiyo ya kula, mara unasikia shinikizo la damu, mara kisukari na mengineyo.

 bad habit2

Hali kadhalika kwenye uvutaji, ulevi na matumizi ya mihadarati, wengi huanza kwa kuonja, baadae kidogo kidogo wanaongeza kiwango mpaka wanafikia kuwa wateja. Kwa mfano uvutaji wa sigara, mtu anakuwa anavuta na anafurahia kwa sababu madhara hayaonekani mara moja, ila baada ya muda yanapoanza magonjwa mbalimbali na saratani ndipo watu huanza kuhangaika kutaka kuokoa maisha yao. Hawakujua kwamba walishaamua wenyewe kuyachezea maisha yao.

  Chochote unachofanya ama unachotaka kufanya angalia madhara ya muda mrefu anayoweza kutokana nacho. Usifanye unafiki wa kufumba macho na kuona ni hali ya kawaida ama matokeo ni ajali ama bahati mbaya. Yapende maisha yako na wapende wanaokuzunguka kwa kuishi maisha yenye maana.

  Angalia tabia ulizonazo sasa na badili mara moja zile zinazoweza kukuetea madhara. Furahia maisha yako.