Kwenye ulimwengu tunaoishi kuna mengi sana yanayotuzunguka. Na kwa kiasi kikubwa mazingira na watu wanaotuzunguka wana mchango mkubwa sana kwetu. Tabia tulizo nazo, ziwe nzuri au mbaya, tumezipata kutoka kwenye mazingira tunayoishi na kwa watu wanaotuzunguka.
Linapokuja swala la maendeleo na kuyafikia malengo yako kuna baadhi ya tabia inabidi uzibadili. Kuna baadhi ya tabia ambazo sio mbaya kwenye jamii ila haziendani na malengo yako. Kwa kuwa na tabia hizo inakuwa ngumu sana kwa wewe kuweza kufikia maengo yako.
Katika kubadili tabia kuna tabia ambazo inabidi kuziacha na kuna tabia ambazo inabidi kijifunza ama kuzichukua. Tabia kama kupenda starehe sana, ulevi, kusema watu, uvivu, wizi, dhuluma na woga unatakiwa kuziacha mara moja ili uweze kufikia malengo uiyojiwekea.
Tabia kama kupenda kujisomea na kuongeza maarifa, upendo, kufanya kazi, kutokata tamaa, kuweka akiba, matumizi mazuri ya fedha na ujasiri inabidi ujifunze na kuzichukua ili kuweza kufikia mafanikio.
Huenda umeshaamua kubadili baadhi ya tabia ama kujifunza tabia mpya ila inakuwia vigumu sana na mara nyingi unajaribu na kuishia kushindwa. Sio kwako tu wengi wamekutana na hali kama hiyo. Unashindwa kwa sababu uikuwa hujui hiki utakachojua hapa leo.
Kwa kuwa tabia zinaambukizwa(tunazipata kutoka kwa wanaotuzunguka), njia kuu ya kuachana na tabia usiyoitaka na kujifunza tabia unayoitaka ni kwa kundoa ama kujenga mahusiano na vitu ama watu wenye tabia kama hiyo. Punguza mahusiano na wale ambao wana tabia unayoiepuna na jenga mahusiano na wale wenye tabia unayojifunza.
Kuondoa tabia ambayo sio nzuri ni vigumu kama utatumia nguvu nyingi kutaka kuiondoa, ila ni rahisi kama ukibadili tabia hiyo na tabia nyingine ambayo ni nzuri. Kwa mfano kama una tabia ya ulevi, tafuta kitu cha muhimu ambacho utakuwa unafanya kwenye muda ambao huwa unaenda kunywa, inaweza kuwa kujisomea, kuandika, kufanya mazoezi ama chochote ambacho unapenda.
Kama una tabia ya kuwasema watu na unashindwa kuiacha ibadili kwa tabia ya kusifia watu. Kwa mfano kama unaongea na mtu na mara linakuja wazo la kuanza kumsema mtu mwingine badala ya kujiumiza kuzuia kusema endelea kwa kumsifia. Hiyo itakusaidia kuondkana na tabia usiyoipenda mara moja.
Kujifunza tabia mpya ni ngumu sana hasa pale ambapo huna malengo ya kwa nini unataka kuwa na tabia hiyo. Ni vyema kuwa na malengo thabiti na kuona vile utakavyokuwa ama maisha yako yatakavyobadilika kwa wewe kuwa na tabia unayotaka kujifunza. Kwa mfano kama unataka kujifunza tabia ya kujisomea na kungeza maarifa, weka malengo ya kusoma vitabu viwili kila mwezi na kwa mwaka unakuwa umesoma zaidi ya vitabu ishirini. Hebu pata picha utakuwa wa aina gani kwa kusoma vitabu ishirini kuhusiana na kazi unayoifanya! Lazima utakuwa umebobea na katika ulimwengu wa sasa waibobea ndio wanaotawala. Fanya hivyo na matunda yake utayaona.(bonyeza hapa kupata mpango mzuri wa kujisomea)
Kama unajifunza tabia mpya, hakikisha unaifanya mara kwa mara mpaka inapokuwa kawaida kwako. Inashauriwa kufanya kitu kitakachokujengea tabia unayotaka kwa siku ishirini na moja mfululizo ili iweze kuwa tabia kwako.
Ukiamua kubadili ama kujifunza tabia yoyote unaweza kama ukitumia njia hizo.