Kama kuna maneno yanayoweza kumuua mtu kifikra na maneno haya mawili, HAPANA na HUWEZI. Maneno haya yanatumika sana katika jamii bila ya watumiaji kujua madhara makubwa ya maneno haya. Kwa wastani mtu mzima ameshaambiwa hapana zaidi ya mara elfu moja katika maisha yake. Kurudiwa rudiwa kwa maneno haya humfanya mtu aamini ni kweli anayoambiwa hivyo kushindwa kufikia ndoto zake.

  Kama hauko imara na kama hujajipanga vya kutosha ni vigumu sana kufikia ndoto zako. Unaweza kuwaambia watu ndoto zako na wengi wakakwambia HUWEZI kufikia kufikia hayo malengo, na watakupa sababu za kutosha kwa nini utashindwa. Unaweza kuwapuuza na kuendelea na mipango yako, ila utakapokutana na changamoto (ni lazima utakutana nazo) yale maneno yao yataanza kukujia na kuamini ni kweli walikuwa sahihi. Utaona zile sababu za kwa nini utashindwa zikijitokeza na hivyo kama hukujipanga vizuri utaacha mara moja.

  Hata wewe mwenyewe umekuwa ukiyatumia haya maneno kwa wenzako kwa kujua au kwa kutokujua. Mara ngapi umemwambia mtu HAPANA kwa ombi ambalo lilikuwa ndani ya uwezo wako kumsaidia? Mara ngapi umemwambia mtu HUWEZI? Hakuna kitu ambach hakiwezekani na huwezi kumpangia mtu ni nini anaweza, ni bora kumwambia mtu hujui ila mpe moyo kwamba akiweka juhudi atafanikiwa.

  Angalia sana watu wa kuwashirikisha ndoto zako maana wengi wana mtazamo hasi na watakurudisha nyuma. Wanaokuzunguka wana ushawishi mkubwa sana kwako na ni rahisi kukubaliana nao kama hujajipanga vya kutosha.

  Kuambiwa HAPANA isikukatishe tamaa, kuambiwa HUWEZI iwe ndio chachu ya kuwaonesha inawezekana. Hakuna mtu anaeweza kukuwekea kikomo, kikomo ni kile unachoweka mwenyewe. Kujipanga ndio jambo la muhimu zaidi, usiingie kichwakichwa.

  KAMA VIONGOZI MAARUFU WA DUNIA NA WANASAYANSI MAARUFU WANGEKUBALIANA NA MANENO HAYA, DUNIA ISINGEFIKA HAPA TULIPO.