Tarehe 31 mwezi wa 12 mwaka 2012 kwenye ukurasa wangu wa facebook niliwashirikisha na kuwashauri watu kwa mwaka huu 2013 wajitahidi wasome vitabu vitatu ambavyo ni THINK AND GROW RICH, POOR DAD RICH DAD na THE RICHEST MAN IN BABYLON. Nilitoa utaratibu kwa watakaovitaka vitabu hivyo kunitumia barua pepe zao na mimi kuwatumia vitabu hivyo kwa barua pepe bila gharama yoyote. Nilipata mwitikio mkubwa sana kwani mpaka mwezi wa kwanza unaisha nilikuwa nimewatumia watu zaidi ya mia mbili(200) vitabu hivyo. Kwa sasa ni miezi mitatu imekwisha tangu nilipowatumia watu vitabu, wachache wamenitumia ujumbe kuniambia jinsi gani walivyojifunza mambo mengi na mapya kutokana na vitabu hivyo. Sijapata mrejesho kutoka kwa wengi, ila ni rahisi tu kutabiri kwamba asilimia kubwa ya watu niliowatumia vitabu vile hawajamaliza kuvisoma na baadhi hawajaanza kabisa kuvisoma. Utaratibu niliokuwa naufikiria ni kwamba kama kwa mwezi mmoja mtu akasoma kitabu kimoja kwa sasa vingekuwa vimeisha na ningeandaa vitabu vingine niwatumie. Ila kwa sababu naona utaratibu huo ni mgumu kwa watu kuufikia nimefikiria utaratibu mwingine ambapo kila mwezi nitawashirikisha na kuwatumia watu kitabu kimoja wakisome.
Vitabu ninavyowashirikisha watu ni vitabu vinavyohusu maisha, maendeleo binafsi, biashara, uchumi, usimamizi wa fedha na mbinu za kutoka kimaisha. Ni vitabu vizuri sana kwani vinakupa mtazamo tofauti wa maisha hasa kwa kipindi hiki ambacho maisha yamekuwa magumu sana. Ni vitabu vizuri sana ambavyo wenzetu wazungu wanavisoma sana na vinawasaidia sana. Sote tunajua utaratibu wa kujisomea vitabu ni mgumu sana kwa watanzania ila ni lazima tubadilike kama tunataka kwenda na kasi ya dunia la sivyo tutaachwa tukishabikia tu vya wazungu na kutegemea misaada.
Naomba maoni yako kuhusu huo utaratibu mpya wa kusoma kitabu kimoja kwa mwezi.
Kwa wale ambao hawakupata vitabu vitatu nilivyotoa mwanzo bonyeza hapa na uandike jina na email yako utatumiwa papo hapo.
NAWATAKIA HERI YA PASAKA WATANZANIA WOTE………..
NAIPENDA TANZANIA.